WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), umewataka wananchi kuchangamkia huduma zinazotolewa na taasisi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma leo Jumanne, Afisa Msajili wa RITA, Nyanda Masunda, amesema shirika lake, limejipanga kutoa huduma ya msaada wa kisheria juu masuala mbalimbali yanayosimamiwa na taasisi hiyo.
Rita – kwa mujibu wa sheria za Tanzania Bara – ndilo shirika lililoruhusiwa kusimamia mirathi, kutunza na kuhifadhi wosia, pamoja na kusajili vyeti vya kuzaliwa.
Ametoa kauli hiyo, kwa lengo la kuwahamisha wananchi waweze kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square, mjini Dodoma.
“Muitikio wa watu bado ni mdogo, hivyo tunawasihi wananchi kujitokeza kwa wingi, kwani RITA ipo hapa na timu nzima ya wanasheria wetu kukupa ushauri wa kisheria juu ya mambo ya mirathi na namna bora ya kuandika wosia na kutunza kumbukumbu,” ameeleza Nyanda.
Aliongeza: “Hii ni fursa kubwa kwa wakazi wa Dodoma na maeneo ya jirani.”
Nyanda amesema, RITA inaendelea kusogea karibu na wananchi ili kuwapa elimu ya wosia na mirathi, lengo ni kupunguza migogoro mbalimbali ya kifamilia na mashauri ya mirathi kwenye mahakama zetu.
Maadhimisho ya siku ya haki za binadamu kitaifa, hufanyika kila tarehe 10 Desemba ya kila mwaka, ambapo mwaka huu kauli mbiu yake ni “Maadili, Hakiza Binadamu, Utawala Bora na Mapambano dhidi ya Rushwa, ni jukumu la pamoja kati ya serikali na wadau wengine.
RITA kama wadau wapo kwa ajili ya kutoa huduma kadhaa, ambazo ni kikwazo katika mapambano katika utetezi wa haki za binadamu.
Leave a comment