Saturday , 27 April 2024
Home Habari Mchanganyiko RC Makalla azindua ‘Mwalimu Spesho’ Dar, atoa ujumbe
Habari Mchanganyiko

RC Makalla azindua ‘Mwalimu Spesho’ Dar, atoa ujumbe

Spread the love

KONGAMANO la Siku ya Walimu na Benki ‘NMB Teachers Day’ Mkoa wa Dar es Salaam, limefanyika na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa (RC), Amos Makalla huku likitumika pia kuzindua Huduma ya Mwalimu Spesho, kifurushi kilichobeba fursa kibao kwa kada hiyo ya watumishi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Uzinduzi wa Mwalimu Spesho – chini ya kaulimbiu isemayo; Umetufunza, Tunakufunza, umefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kardinali Rugambwa, Oysterbay, ukishirikisha zaidi ya walimu 500 kutoka wilaya za Kinondoni, Ubungo, Temeke, Kigamboni na Ilala.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla (katikati) akizungumza na Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (kulia) na Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard wakati wa siku ya walimu mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza kabla ya RC Makalla kuzindua Kongamano hilo jana Jumanne tarehe 26 Julai 2022, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, alisema kwa mwaka wa 10 mfululizo, benki yake imekuwa na utaratibu wa kukutana na walimu, ili kuthibitisha umuhimu na thamani ya kundi hilo kwa maendeleo ya taifa na ustawi wa NMB.

“Kupitia NMB Teachers Day, tumekuwa tukibadilishana mawazo na walimu, hii ni benki yao na tunakutana nao kupokea maoni yao juu ya huduma zetu na kuyafanyia kazi. Lakini leo kutokana na upekee wa kada hii, tukaona tuwatengenezee ‘package’ maalum iitwayo Mwalimu Spesho, kifurushi ambacho ndani yake kuna faida mbalimbali.

“Ndani ya Mwalimu Spesho kuna mikopo mbalimbali ya riba nafuu, ikiwemo ya elimu kwa walimu wenyewe na watoto wao ikiwa na riba ndogo ya asilimia 10, pia kuna mikopo ya kilimo kwa walimu wanaojihusisha nacho, pia ipo mikopo ya pikipiki na bajaj kwa ajili ya kutanua mifumo ya kibiashara na usafiri kwa wakopaji,” alibainisha Mponzi.

Aidha, aliongeza Mwalimu Spesho pia inajumuisha droo ndogondogo kwa walimu, ambazo zimekuwa zikitoa zawadi ya vyombo vya ndani kama friji, tv, sambamba na semina elekezi zinazotumika kutoa elimu ya fedha kwa ustawi wa biashara zao na maisha yao kwa ujumla wawapo kazini na hata baada ya kustaafu.

Kwa upande wake, RC Makalla aliliita Kongamano hilo kuwa ni jambo jema linalopaswa kuigwa na taassisi zingine nchini, ili kuwaongezea walimu nafasi ya kukua kibiashara na kiuchumi, huku akiipongeza NMB kwa mipango endelevu na yakinifu katika kuwafikia walimu zaidi ya 5,000 kote nchini, ambao ni sehemu tu ya wanaounda kada hiyo ya utumishi.

“Walimu ni kati ya kada yenye watumishi wengi zaidi wa Serikali, kulifikia, kulielimisha na kuliongezea fursa kundi hili ni kutekeleza kwa vitendo na kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akitoa maelekezo na kusisitiza umuhimu wa kusapoti kada zote za watumishi, wafanyabiashara wadogo na hata makundi maalum.

“Wito wangu kwenu NMB, makongamano haya yasiishie kwa walimu tu, bali yaende mbali zaidi na kuyafikia makundi mengine ya watumishi wa Serikali na jamii, pamoja na kubuni bidhaa na huduma rafiki kwao. Mkoa wangu wa Dar es Salaam una Watendaji wa Mita 520 na Watendaji wa Kata 170, hawa nao wanahitaji kufikiwa nanyi NMB,” alisisitiza Makalla.

Makalla aliwakumbusha walimu Falsafa ya ‘I=2C+S’ aliyowapa walimu katika kongamano lililopita (yaani ‘Income Can be Consumed or Saved’) inayosisitiza umuhimu wa matumizi yanayozingatia uwekaji akiba katika pato la mtu yeyote, huku akiwaongezea Falsafa mbili kwa maisha yao baada ya kustaafu, ambazo ni Bima ya Maisha na Utendaji na Umri.

“Bima ya maisha itawasimamia baada ya kustaafu, maana yangu hapa ni kwamba mpange na kuchagua mifumo rafiki itakayolinda maisha yenu nje ya ajira zenu. Ijue, ipange na chagua ‘future’ ya maisha yako leo, kupitia NMB. Pia lazima mtambue umri unaamua jambo la kufanya, hivyo kadri unavyosonga, unapaswa kupunguza mambo ya kufanya kwa ustawi wa maisha yenu ya baadaye,” alisema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!