August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Kisena, wenzake yatua Mahakama ya Mafisadi

Spread the love

 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam – Kisutu imefunga jalada la kesi mbili kati ya tatu za uhujumu uchumi zinazomkabili mkurugenzi wa mradi wa Usafirishaji wa Mabasi yaendayo haraka, maarufu kama mwendokasi (UDART), Robert Kisena na wenzake na kutoa amri ya kuhamishiwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ambako ndiko itakakosikilizwa na kuamuriwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa Mashtaka kukamilisha upelelezi na kuwasomea washtakiwa maelezo ya ushahidi na vielelezo. Anaripoti Erick Mbawala na Juliana Assenga, Dar es Salaam … (endelea).

Katika kesi namba 20, iliyokuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwenye hatua ya uchunguzi wa awali, Kisena na wenzake kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 15.

Mbali na Kisena (47) ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni ya Simon Group Ltd, washtakiwa wengine ni Charles Newe (48) mkurugenzi wa Udart, mfanyabiashara John Samangu ( 66) na Mhasibu wa Udart, Tumaini Kulwa ( 44).

Mashtaka hayo yanayowakabili ni pamoja na kuongoza genge la uhalifu, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo, utakatishaji fedha haramu na kuisababishia Udart hasara ya Sh750, milioni, wakidaiwa kutenda makosa hayo kati ya tarehe 25 Mei na 10 Julai, 2016.

Awali Mawakili wa Serikali, Ladislaus Komanya, Tumain Mafuru na Timotheo Mmari leo tarehe 27 Julai, 2022 wameieleza mahakama hiyo kuwa katika shauri hilo wanatarajia kuwaita mashahidi 24 na kuwasilisha vielelezo 58.

Mawakili hao wa Serikali wakiongozwa na Wakili Mwandamizi, Ladislaus Komanya wamesema tayari wameshawasilisha taarifa za maelezo hayo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa hatua zaidi.

Amesema vielelezo hivyo vitajumuisha nyaraka mbalimbali ikiwemo mikataba, hati za makubaliano, hati za kuamuru utoaji wa vielelezo, taarifa ya ukaguzi wa hesabu, nyaraka za benki na hati za uthamini.

Aidha, katika ya kesi ya pili iliyokuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo yak Kisutu, Godfrey Isaya, mawakili wa Serikali wakiongozwa na Ladislaus Komanya wameieleza mahakama hiyo kuwa katika shauri hilo kutakuwa na jumla ya mashaidi 30 na vielelezo 96.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Isaya pia amewaeleza watuhumiwa kuwa wataendelea kuwa mahabusu mpaka pale shauri hilo litakapoitishwa kwenye Mahakama Kuu divisheni ya Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi (Mahakama ya Mafisadi).

Katika kesi hiyo ya pili namba 21, iliyokuwa ikisikilizwa na  Isaya, mbali na Kisena washtakiwa wengine ni Charles Newe ( 48) mkurugenzi wa Udart; mfanyabiashara John Samangu ( 66); mtunza fedha wa Udart,  Tumaini Kulwa  ( 44) na mkurugenzi wa kampuni ya Maxcom Africa, maarufu kwa jina la kibiashara la Maxmalipo, Juma Furaji (48).

Kisena na wenzake wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 22 ya kuongoza genge la uhalifu, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo, utakatishaji fedha haramu na kuisababishia Udart hasara ya Sh bilioni 4.5.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti Kati ya Juni 2015 na tarehe 30 April, 2016.

Wanadaiwa kuwa walihamisha fedha hizo kutoka katika akaunti ya Udart katika benki ya NMB, tawi la Bank House, kwenda akaunti ya kampuni ya Long Way Engineering Ltd iliyoko Benki ya KCB.

error: Content is protected !!