August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge amuangukia Samia ujenzi barabara kuelekea Burundi

Mbunge wa Jimbo la Buyungu, wilayani Kakonko, Mkoa wa Kigoma, Aloyce Kamamba

Spread the love

 

MBUNGE wa Buyungu, wilayani Kakonko, Mkoa wa Kigoma, Aloyce Kamamba, ameiomba Serikali itoe fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara inayounganisha mkoa huo wa nchi jirani ya Burundi, kupitia mpaka wa Muhange. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kamamba ametoa ombi hilo jana tarehe 27 Julai 2022, katika kikao chake na wananchi wa Jimbo la Buyungu waishio jijini Dar es Salaam, alichokiitisha kwa ajili ya kuwaeleza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali jimboni humo.

Mbunge huyo amesema kwa sasa Burundi imehamisha makao makuu yake kutoka Bujumbura kuja Gitega, mji uliokaribu na Kakonko, hivyo ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami utaimarisha mahusiano ya kibiashara na kijamii kati ya Kigoma na nchi hiyo.

“Tunaendelea kumuomba Rais Samia kupata barabara inayotuunganisha sisi Kigoma na Burundi, kupitia Wilaya ya Kakonko. Ni ukweli Burundi wamehamisha makao makuu ya nchi kutoka Bujumbura kuja Gitega, kutoka mpaka wa Muhange kwenda makao makuu hayo ni karibu,” amesema Kamamba.

Kamamba amesema “kupata barabara kutoka Kakonko kwenda mpaka wa Muhange ni fursa. Tutaendelea kufuatilia Serikali kutupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutuunganisha na Burundi.”

Mbali na ombi hilo, Kamamba ameiomba Serikali ya Rais Samia, kuunga mkono jitihada za wananchi wa Wilaya ya Kakonko za kujenga shule maalum ya wasichana, kwa kuhakikisha inakuwa na madarasa ya kidato cha tano na sita.

“Tumeboresha yaliyokuwa majengo kwa ajili ya shule maalum ya watoto wa kike. Tunajua wana changamoto nyingi wamepelekwa pale na tumeomba Serikali ituunge mkono, ituwekee kidato cha tano na sita ili watoto wengine waje waungane na watoto wetu waweze kuwatia joto na nguvu wafanye vizuri,” amesema Kamamba.

Akielezea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Rais Samia jimboni kwake, amesema kwa sas ainajenga Hospitali yua Wilaya ya Kakonko, vituo vya afya katika kata mbili ikiwemo ya Gwarama. Pamoja na zahanati katika vijiji vitano ikiwemo cha Rumashi, Njomlile, Kihomoka na Usenga.

Kuhusu elimu, Kamamba amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh. 600 milioni kwa ajili ya ujenzi wa shule za Sekondari.

“Kuna shule Rais Samia ametuletea Sh. 600 milioni na tayari katika hizo Sh. 470 milioni zimeletwa Kata ya Katanga. Kuna Sekondari tunajengewa katika Kijiji cha Kaziramihunda inaitwa Dk. Mpango. Kuna sekondari inajengwa Kakonko inaitwa Ikambi,” amesema Kamamba.

Aidha, Kamamba amesema, kwa sasa Serikali inawawezesha wananchi wa jimbo lake katika masuala ya kilimo, hasa cha alizeti na michikichi.

Kwa upande wa wananchi walishiriki kikao hicho, wamempongea Kamamba kwa hatua hiyo wakisema inalenga kuwashirikisha wananchi katika masuala yanayohusu maendeleo yao.

Dalius Kalijongo, alimuomba Kamamba aiombe Serikali ifikishe umeme katika vijiji ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo, ikiwemo kijiji cha Ruamashi ambacho kina shughuli nyingi za biashara na kilimo cha mpunga, mihogo na mtama.

Naye RoseMarry Katunzi, alimuomba Kamamba asimamie suala la uwezeshaji kiuchumi wanawake na vijana , kupitia mikopo inayotolew a na Halmashauri.

error: Content is protected !!