Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Samia, Mbatia wavutana ongezeko kodi ya mafuta
Habari za Siasa

Rais Samia, Mbatia wavutana ongezeko kodi ya mafuta

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi
Spread the love

 

WAKATI Rais Samia Suluhu Hassan, akisema Serikali imeongeza kodi ya Sh. 100 kwa kila lita moja ya mafuta, ili ipate fedha za ujenzi wa miundombinu, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amepinga hatua hiyo akisema itadumaza ukuaji uchumi wa nchi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Viongozi hao wametoa kauli hizo leo Alhamisi, tarehe 8 Julai 2021, katika nyakati tofauti. Rais Samia aliitoa katika ziara yake mkoani Morogoro, wakati Mbatia akitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, akizungumza na wanahabari.

Akizungumza na wananchi wa Morogoro, Rais Samia amesema hatua hiyo ya Serikali kuongeza kodi ya mafuta imeleta kelele, lakini lengo lake ni kuhakikisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), unapata fedha za kutosha kujenga barabara.

“Kuna suala la barabara za vijijini ziko chini ya Tarura, niwape taarifa kwamba tumeongeza fedha kidogo kwenye mafuta. Pengine mmesikia kelele kelele za mafuta, lakini tumeongeza Sh. 100 kwenye kila lita ya mafuta, ili tuweze kukusanya fedha zikatusaidie kujenga barabara vijijini,” amesema Rais Samia.

https://www.youtube.com/watch?v=Z-jaTasHG0k

Katika bajeti yake kuu kwa mwaka wa fedha wa 2021/22, Serikali imeongeza ushuru wa barabara kwa Sh. 100 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli, ili ipate fedha za ujenzi na ukarabati wa barabara za vijijini kupitia Tarura.

Kupitia ushuru huo, Serikali inatarajia kupata zaidi ya Sh. 322 bilioni.

Rais Samia amesema, fedha hizo zitapelekwa Tarura pamoja na kutumika katika kuimarisha masuala ya ufundi na teknolojia ya ujenzi wa miundombinu ya barabara hasa za vijijini.

“Kwa maana hiyo tunakwenda kuiongezea fedha Tarura na ufundi, aina ya barabara za kujenga vijijini ili zitakapojengwa ziweze kukaa muda mrefu. Sababu tumepoteza fedha nyingi kujenga barabara vijijini, mvua zikipiga zinaondoka shida inarudi,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Kwa hiyo tunakwenda kubadilisha ufundi au teknolojia , ili barabara zetu vijijini ziweze kuishi muda mrefu.”

Awali, Mbatia amesema hatua hiyo imepandisha bei ya mafuta, hali itakayoathiri uchumi wa nchi.

“Leo tumeshuhedia bei ya mafuta ni kubwa sana na inaenda kwa kasi kubwa sana, mfano bei ya lita moja ya petroli kiuhalali ikifia bandarini ni Sh. 1,162, lakini ukienda kwenye vituo unanunua bei hiyo kwa Sh. 2,405, zaidi ya mara mbili na hii sababu gani? Kuna kodi nyingi mno, kwenye mafuta kuna kodi zaidi ya 20,” amesema Mbatia na kuongeza:

“Hatua hii kwenye athari za uchumi ni kubwa mno, sababu shughuli zote zinategemea mafuta na Taifa linangia hasara sababu kwenye usafirishaji bidhaa zinategemea mafuta. Huduma ya usafirishaji bidhaa na mazao zitakuja juu, uzalishaji wa bidhaa utakuja juu pia, anayeumia ni Mtanzania.”

1 Comment

  • Sasa tutegemee ongezeko katika gharama za usafirishaji – kuanzia daladala hadi bajaji,teksi na mabasi ya mkoani. Mzigo kwa mwananchi masikini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

error: Content is protected !!