HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma, nchini Tanzania, limemaliza mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 kati ya halmashauri hiyo na wafanyabiashara wa soko la Sabasaba. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Mgogoro huo umepatiwa ufumbuzi baada ya Naibu Meya wa halmashauri ya Jiji, Emmanuel Chibago na Afisa Biashara wa Jiji, Donatila Vedasto kukaa vikao vya mara kwa mara ambavyo vilikuwa vikilenga kujenga mahusiano mazuri hususani katika suala zima la ulipaji kodi.
Katika mkutano wa pamoja uliofanyikia katika ofisi ya soko la sabasaba kwa kuwashirikisha viongozi wa Jiji na wafanyabiashara, Donatila alisema, umefika wakati sahihi sasa kwa wafanyabiashara wa soko la sabasaba kulipa kodi kwa faida ya uboreshaji wa soko hilo.
“Ndugu zangu wafanyabiashara wa sabasaba, tumekuwa tukifanya mikutano na vikao mara kwa mara ili kutafuta ufumbuzi wa kulipa kodi ndani ya soko letu la sabasaba.”
“Na kulipa kodi ni pamoja na kujisajili ili kila mfanyabiashara aweze kufahamika na aina ya biashara anayoifanya kwa kufanya hivyo kutasaidia kuwatambua na wale ambao watakuwa wamejisajiri kwa vyovyote vile yanapotokea maboroshe watu hao watapewa kipaumbele tofauti na wale ambao bado hawajajisajiri”alieleza Donatila.
Naye Naibu Meya Chibago, aliwaambia wafanyabiashara hao wa soko la sabasaba ili nchi iweze kupiga hatua ni lazima kodi ilipwe kwa maendeleo ya nchi.
“Wafanyabiashara wa sabasaba tumekuwa tukizungumzia ulipaji wa kodi, ukweli ni hatuwezi kukwepa ulipaji wa kodi katika eneo hill la wafanyabiashara lakini pia uongozi wa halmashauri ya Jiji hauwezi kukaa peke yao na kupanga kodi ambayo mnatakiwa bali kinacho fanyika ni kushirikishana na kufikia mwafaka kama ilivyofanyika katika mkutano huu,” alisema Chibago.
Kwa upande wake, mmoja wa wafanyabiashara, Steven Masawe alisema wafanyabiashara hawana tatizo na ulipaji wa kodi ili mradi tu uwekwe utaratibu unaotakiwa.
Leave a comment