July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe apata pigo, kaka yake afariki kwa Covid-19

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amepata pigo baada ya kuondokewa na kaka yake, Charles Mbowe, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo tarehe 8 Julai 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Akitangaza msiba huo, Mbowe amesema Charles amefariki dunia kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na Virusi vya Corona (Covid-19), katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC, Moshi  mkoani Kilimanjaro, alikokuwa  anapatiwa matibabu.

“Ndugu Watanzania wenzangu, familia yetu ya kina Mbowe imepata msiba mkubwa wa kaka yetu Charles, ambaye amefariki kwa ugonjwa wa Covid-19 katika Hospitali ya KCMC, usiku wa kuamkia leo,” amesema Mbowe.

Mwenyekiti huyo wa Chadema amesema, mazishi yatafanyika kijijini kwao Machame mkoani Kilimanjaro, Jumatatu tarehe 12 Julai mwaka huu “mazishi yatafanyika kijijini Machame siku ya Jumatatu, kuanzia saa saba mchana.”

Mbowe amesema mazishi ya Charles yatakuwa binafsi, ili kukwepa msongamano wa watu kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya Covid-19.

“Kutokana na ukweli kwamba kuna maambukizi ya Covid-19,  tunawaomba Watanzania walioonesha nia ya kujumuika na sisi, kwa wingi wao tuwaombe wachukue tahadhari zote za kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Covid-19. Tuepuke mikusanyiko isiyo ya lazima,” amesema Mbowe. 

Mbowe ameongeza “tunawapenda wote wabaki hai wasiambukizwe. Taratibu za mazishi zitakuwa tofauti. Tutakuwa na utaratibu binafsi ndugu wa karibu sana watashiriki katika utaratibu wa kumzika Charles.”

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Kufuatia msiba huo, Mbowe alilazimika kusisitiza ziara yake ya ujenzi wa Chadema, visiwani Zanzibar.

“Nimelazimika kusitisha ziara yangu katika Visiwa vya Zanzibar, ili kuweza kuja kushirki na familia katika msiba,” amesema Mbowe.

error: Content is protected !!