Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Samia ateta kimtandao na bosi EU
Habari za Siasa

Rais Samia ateta kimtandao na bosi EU

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amezungumza kwa njia ya mtandao na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Charles Michel. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mazungumzo hayo yamefanyika, leo Jumatatu, tarehe 12 Julai 2021, Ikulu jijini Dodoma ambapo viongozi hao wawili wamezungumzia masuala yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na umoja huo.

Michel amempongeza Rais Samia kwa hatua mbalimbali anazochukua tangu kushika hatamu ya uongozi na kumhakikishia kuwa Umoja wa Ulaya (EU) utaendelea kuwa mshirika muhimu na wa kimkakati wa maendeleo nchini Tanzania na kikanda.

Aidha, Michel amempongeza pia kwa jitihada anazochukua kupambana na ugonjwa wa Corona.

Vilevile amemueleza kuwa EU tayari inashirikiana na viwanda mbalimbali vinavyozalisha chanjo barani Afrika kwa kuvijengea uwezo na kuongeza kuwa iwapo Tanzania itahitaji msaada huo EU iko tayari kuisaidia.

Kwa upande wake, Rais Samia ameshukuru Umoja wa Ulaya (EU) kwa ushirikiano katika masuala ya maendeleo ya jamii na kuwekeza katika miradi ya miundombinu kupitia Benki ya Uwekezaji ya EU.

Rais Samia amesema benki hiyo imetoa Euro milioni 50 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa baadhi ya viwanja vya ndege vya mikoani.

Amesema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita Tanzania na Umoja wa Ulaya zimesaini makubaliano ya msaada wa Euro milioni 111.5 kwa ajili ya kuboresha miradi ya sekta ya nishati hususani matumizi ya majiko banifu, uongezaji thamani mazao ya nyuki, kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha usalama wa chakula.

Rais Samia amesema kwa sasa Serikali inaendelea na uboreshaji wa mazingira bora ya uwekezaji kwa sekta binafsi ili kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) wa Tanzania.

Aidha, Rais Samia amemhakikishia Michel kuwa utawala wake utasimamia na kuimarisha demokrasia, utawala bora na haki za msingi za binadamu.

Kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, Rais Samia amemtaarifu Rais huyo kuwa Tanzania tayari imeshajiunga na Mpango wa Kimataifa wa ugawaji wa chanjo kwa nchi masikini (COVAX facility) na ina mpango wake wa taifa wa kupambana na Corona unaoainisha mahitaji ya nchi hivyo itawasilisha mahitaji yake kwa EU ili kupata msaada.

Rais ameshukuru kupokea mualiko wa kutembelea Umoja wa Ulaya na kumtumia salamu Rais wa Umoja huo, Ursula von der Leyen.

Taarifa ya mazungumzo hayo, imetolewa na Jaffar Haniu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!