RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa mchango mkubwa wa Serikali yake katika uboreshaji huduma za afya kwenye Jimbo la Musoma Vijijini, mkoani Mara. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mara … (endelea).
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Abdalla Shaibu Kaim, akikagua utekelezaji wa miradi ya sekta ya afya, jimboni humo, ambaye aliambatana na timu yake.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, imesema amewapongeza viongozi wa jimbo hilo pamoja na wananchi kwa kazi kubwa wanayofanya kuanza utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa nguvu zao, kisha kuungwa mkono na Serikali.
“Kaim na timu yake yote wameipongeza sana Serikali na Rais Samia , kwa kutoa michango mikubwa ya kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Musoma Vijijini. Vilevile, Wananchi na viongozi wao wa Chama na Serikali Musoma Vijijini wamepongezwa kwa kazi nzuri wazifanyazo kwenye utekelezaji ya miradi ya maendeleo ya vijijini mwao,” imesema taarifa hiyo.
Miongoni mwa miradi ambayo wananchi wa jimbo hilo wanashirikiana na Serikali kuitekeleza ni hospitali moja ya hadhi ya wilaya, katika Kitongoji cha Kwikonero, vituo sita vya afya, zahanati 41.
Pia, mbunge wa jimbo hilo, Prof. Muhongo amegawa magari matano ya kusafirishia wagonjwa (Ambulances).
Leave a comment