Friday , 3 May 2024
Home Kitengo Habari Kimataifa Rais Ruto aanza na bandari Mombasa, mbolea, majaji
KimataifaTangulizi

Rais Ruto aanza na bandari Mombasa, mbolea, majaji

Spread the love

 

SAA chache baada ya kuapishwa kuwa Rais wa tano wa Kenya, Dk. William Ruto ameonekana kuanza kazi kwa kasi ya ajabu, baada ya kutoa amri ya kurudishwa kwa shughuli za bandari ya Mombasa.

Pia ametangaza kupunguza bei ya mbolea kutoka Ksh 6,500 (Tsh 126,000) hadi Ksh 3,500 (Tsh 68,000) kwa mfuko wa kilo 50 pamoja na kutangaza kuteua majaji sita wa mahakama ya rufaa, waliokataliwa na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Rais huyo mpya wa Kenya ametoa kauli hiyo leo tarehe 13 Setemba, 2022 wakati akihutubia kwa mara ya kwanza maelfu ya wakenya, viongozi na marais wa nchi za Afrika waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwake zilizofanyika katika uwanja wa kimataifa wa Moi, Kasarani Nairobi.

Mbali na Rais Ruto pia Naibu wake, Rigathi Gachagua naye ameapishwa kuanza kutekeleza majukumu yake.

BANDARI MOMBASA

Akizungumzia kuhusu kurejeshwa kwa shughuli za bandari ya Mombasa, Ruto amesem leo jioni atatoa taarifa zaidi jinsi mchakato huo utakavyofanyika.

Hatua hiyo imeonekana kuwa ameanza kutimiza ahadi zake hasa kwa watu wa Pwani ya Kenya ambapo katika kipindi cha kampeni zake mara wa mara alikuwa akisikika akiahidi kwamba uongozi wake utarejesha shughuli za bandari ya Mombasa.

Katika hotuba yake ya kwanza kama rais, Ruto alizungumzia mambo mengi na kusisitiza kwamba mengine yanaanza jioni hii, hilo la Bandari likiwa mojawapo ambalo atalishughulikia pindi atakapoingia kwenye ofisi ya rais baada ya kumalizika kwa hafla ya kuapishwa kwake katika uwanja wa Kasarani.

“Jioni ya leo nitatoa maagizo ya kuidhinishwa kwa bidhaa ili kurejea katika bandari ya Mombasa kama nilivyotoa ahadi. Hii itarejesha maelfu ya kazi kwa wakazi wa Mombasa,” Ruto amesema.

BEI YA MBOLEA

Akizungumzia kuhusu suala la mbolea, Ruto amesema bei ya bidhaa hiyo itaanza kutumika wiki ijayo wakati utawala wake unapoanza safari ya kuboresha sekta ya kilimo nchini.

“Kwa mvua hii ndogo iliyonyesha, tayari tumefanya mpango wa kuagiza mifuko milioni 1.4 ya mbolea kupatikana kwa shilingi 3,500 kutoka kwa bei ya shilingi 6,500 kwa mfuko wa kilo 50,” Ruto amesema.

Rais Ruto vilevile amewaonya wafanyabiashara wanaoficha mbolea kwa lengo la kuzidisha mfumuko bei ya bidhaa hiyo ndipo waiuze.

Kiongozi ametaka serikali za kaunti kuhakikisha kuwa mbolea hiyo inapatikana kwa wakulima nchini.

“Mbolea hii itaanza kupatikana kuanzia wiki ijayo. Ninahimiza serikali za kaunti katika maeneo ya Kati, Mashariki na Magharibi kufanya kazi nasi ili kuhakikisha kuwa mbolea hii ipo ili tuanze safari yetu ya kuimarisha uzalishaji wa chakula nchini,” Ruto amesema.

ATEUA MAJAJI WALIOTEMWA NA KENYATTA

Aidha, katika kile kinachodhihirisha kuanza kwa zama mpya, Ruto ametangaza kuteua majaji sita wa mahakama ya rufaa, waliokataliwa na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta.

Rais huyo amesema atasimamia kuapishwa kwao kesho Jumatano.

Majaji sita ambao Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alikataa kuwateua licha ya Tume ya Idara ya Mahakama (JSC) kuwapendekeza ni George Odunga, Aggrey Muchelule, Joel Ngugi na Weldon Korir, pamoja na hakimu mkuu Evans Makori na naibu msajili wa Mahakama Kuu Judith Omange.

Uhuru Kenyatta

Aidha, majaji hao sita ni miongoni mwa majaji 40 waliopandishwa madaraka na JSC Juni 2021 lakini Rais Kenyatta alikataa kuwateua licha ya amri ya Mahakama Kuu.

“Kesho (Jumatano), nitasimamia kuapishwa kwao waanze kuhudumia Wakenya,” Dk. Ruto amesema.
Rais huyo wa tano wa Jamhuri ya Kenya, vilevile ametangaza nyongeza ya mgao wa bajeti kwa idara ya mahakama.

KUFUNGUA MILANGO

Rais huyo pia ameahidi kufungua fursa za mafanikio kwa wananchi wa taifa hilo.

“Ninaahidi kufungua kila mlango wa fursa na kuacha wazi kila mlango hadi mafanikio yatakapopatikana na viongozi wengine mfanye kama hivyo, ili kwa pamoja tutanue fursa na nafasi kwa wananchi wetu,” amesema Ruto.

Pia ameahidi kuwa Serikali yake itafungua fursa za ajira, pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, pamoja na kuandaa maeneo rasmi katika miji na majiji nchini humo kwa ajili ya wananchi kufanya biashara.

Ameongeza kuwa Serikali yake itaimarisha utendaji wa taasisi za umma kwa kuhakikisha zinajitegemea kiuchumi, hasa mahakama, Jeshi la Polisi, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Sabaya afutiwa kesi, ruksa kugombea uongozi

Spread the loveMwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP leo Ijumaa amefuta rufaa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kwafukuta kisa chaguzi, Lissu aibua tuhuma nzito

Spread the loveCHAGUZI za kusaka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga “HIDAYA” chaendelea kuimarika, wananchi wapewa tahadhari

Spread the loveMAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

error: Content is protected !!