RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Hussein Mwinyi, amesema 2022 hakutakuwa na sherehe za kitaifa za maadhimisho ya miaka 59 ya mapinduzi ya visiwa hivyo, badala yake fedha zilizopangwa kutekelezea shughuli hizo, zitapelekwa kwenye sekta ya elimu.Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar…(endelea).
Rais Mwinyi ametoa uamuzi huo leo Jumamosi, tarehe 31 Desemba 2022, akitangaza ratiba ya wiki ya maadhimisho ya miaka 59 ya mapinduzi ya Zanzibar, itakayoanza tarehe 1 hadi 12 Januari 2023.
“Mwaka huu kama Serikali tumeamua Serikali kupeleka fedha zilizopangwa kwenye kilele cha sherehe za mapinduzi mwaka huu katika sekta ya elimu ili skuli zetu ziwe na vifaa vya kutosha kuanzia madawati, maabara na maktaba ili tunapokuwa tunazindua skuli nyingi na madarasa mengi, si vyema ziwe hazina dhana zinazotakiwa,” amesema Rais Mwinyi.
Mbali na sababu hiyo, Rais Mwinyi amesema sababu nyingine ya kuahirisha sherehe hizo, ni kujipanga kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 60 ya mapinduzi ya Zanzibar.
“Siku ya kilele huwa tunakuwa na gwaride katika uwanja wa Amani, safari hii haitakuwepo sababu tumeona Serikali tujipange katika maadhimisho kwa jambo kubwa zaidi mwaka ujao ambapo mapinduzi yetu yatafikia miaka 60. Sherehe zitakuwa kubwa zaidi na mambo mengi kuliko kawaida. Kwa maana hiyo Serikali itajipanga kibajeti ili kuweza kutimiza maadhimisho ya mwaka ujao,” amesema Rais Mwinyi.
Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi amesema kwenye wiki ya maadhimisho ya sherehe za mapinduzi, miradi takribani 55 itazinduliwa. Hata hivyo, hakutaja kiasi cha fedha ambacho kitapelekwa katika sekta ya elimu.
Leave a comment