November 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Dk. Mwinyi apongeza utatuzi kero za Muungano, azungumza na Majaliwa

Spread the love

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza mafanikio yaliyopatikana katika vikao vya Muungano ikiwa ni pamoja na kutatuliwa kero kadhaa za Muungano.  Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Rais Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo tarehe 8 Januari, 2022 wakati akizungumza na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipofika Ikulu jijiji Zanzibar kwa mazungumzo.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi amepongeza usimamizi mzuri wa vikao hivyo vya Muungano ambavyo vimeleta tija na kutatua mambo kadhaa ambapo kati ya hoja 18 tayari hoja 11 zimeshapatiwa ufumbuzi na kwa zile zilizobaki ufumbuzi wake utapatikana ndani ya muda mfupi ujao.

Rais Dkt. Mwinyi ametoa salamu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mzuri uliopo, hatua ambayo imekuwa na maslahi mazuri kwa pande zote mbili ikiwa ni pamoja na mgao wa fedha za mkopo wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), ambao utasaidia kuboresha huduma za jamii.

Amesema kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa na msaada mkubwa katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeridhika na hatua ya ushirikiano unavyokwenda hali ambayo itasaidia kuimarisha na kukuza uchumi kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Dkt. Mwinyi ametoa shukrani kutokana na nchi kuwa na amani na utulivu na kusema kwamba hatua hiyo ndio inayopelekea kuimarika kwa uchumi na kueleza kwamba kwa upande wa Zanzibar, utulivu umepatikana na wananchi wanashirikiana vyema na hivi sasa kuna kila sababu ya kupiga hatua kimaendeleo.

Ameeleza athari za UVIKO -19 zilivyoathiri uchumi wa Zanzibar na kueleza jinsi dalili za kuongezeka kwa watalii na kueleza haja ya Zanzibar kujifunza katika ukusanyaji wa mapato hasa baada ya janga hilo la maradhi kutokana na uchumi wa Zanzibar kuwa tegemezi kwa utalii.

Naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amempongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kupata fursa ya kuiongoza Zanzibar hali ambayo anastahili.

Amesema ameanza vizuri kuongoza kwani nchi imetulia na uhusiano wa Wazanzibari umezidi kuimarika.

Amepongeza jinsi Rais Dk. Miwnyi wanavyoshirikiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan na kuahidi kwa upande wao wasaidizi wataendelea kupokea maelekezo yao na kusimamia majukumu ya kuwatumia Watazania wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa jitihada zake za kuimarisha uchumi na hasa katika kuitumia fursa ya Uchumi wa Buluu ambao ni uchumi wa Buluu na kuweka nguvu katika uchumi huo na kueleza kwamba kwa upande wa Tanzania Bara nayo itapanua wigo kutokana na Sera hiyo aliyoiweka Dkt. Mwinyi katika uchumi.

Waziri Majaliwa amemuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kwamba juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha vikao vya Muungano vinaleta tija na kuweza kuondoa changamoto zilizopo kwa haraka.

Amemuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kwamba mamla za ukusanyaji wa kodi zitahakikisha zinakusanya kodi bila ya kutumia nguvu kwa lengo la kuwajengea imani Watanzania kwa Serikali yao pamoja na kuwaamini viongozi wao wote ili nchi izidi kupata mafanikio.

error: Content is protected !!