Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rafu uchaguzi CCM zatamalaki
Habari za Siasa

Rafu uchaguzi CCM zatamalaki

Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Spread the love

RAFU katika uteuzi wa wajumbe watakaogombea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), zimetamalaki. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Akizungumza na wanahabari leo tarehe 21 Oktoba 2019 jijini Dar es Salaam, Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM, ameagiza mchakato wa kura za maoni urudiwe katika maeneo yenye rafu hizo.

Dk. Bashiru ameagiza mchakato wa kura za maoni urudiwe kabla ya tarehe 31 Oktoba 2019, huku akielekeza wanachama wote waliogombea awali,  kuchaguliwa kwa kura za maoni, bila kupitia kwenye hatua ya mchujo.

“Kuna maeneo kulikuwa na mvutano na fujo, nako huko uchaguzi urudiwe, kote hakutakuwa na mchujo tena. Wagombea wote warudishwe hata kama walikuwa 40 wapigiwe kura ya maoni.

Mchakato wa ndani utaongezwa kwa siku mbili zaidi, ilikuwa tumalize tarehe 29 sasa tunaongeza siku 2 mpaka 31, baada ya hapo tuwe tumepata wagombea,” amesema Dk. Bashiru.

Katibu Mkuu huyo wa CCM ametoa agizo hilo akisema kwamba, mchakato wa kura za maoni uliofanywa hivi karibuni, ulikuwa na dosari katika baadhi ya maeneo.

Dk. Bashiru amesema dosari hizo zimesababisha malalamiko kutoka kwa wapiga kura, sambamba na uteuzi wa wagombea wasio na sifa.

Dk. Bashiru ametaja kasoro hizo kuwa ni, ukiukwaji wa kanuni ya uteuzi ya CCM, kutotumika kwa vituo vilivyopangwa, kuchelewa kwa upigaji kura za maoni, rushwa na upendeleo, pamoja na uteuzi wa wagombea wasiokuwa na sifa.

“Yako maeneo ambayo hayakuzingatia kanuni, tunayo kanuni ya uteuzi ndani ya chama chetu, inayoelekeza utaratibu wa kupata wagombea, kuwachuja, kuchukua fomu, kupiga kura za maoni na kuteua. Baadhi ya maeneo hayakuzingatia kanuni, “ ameeleza Dk. Bashiru na kuongeza;

“Yako pia maeneo ambayo hapakuwepo na maelewano, na wakati mwingine yalikuwepo mabishano na kutoridhishwa na mchujo na kura za maoni zilizofanyika. Baadhi ya maeneo migongano hiyo imezuia mchakato kuendelea au baadhi ya wapiga kura kususa au kukaa kando.”

Dk. Bashiru ameeleza kuwa “Tatizo la kukosekana kwa uwazi katika uhakiki, nani ana sifa ya kupiga kura ya maoni zilijitokeza. Kulikuwa na madaftari yameandaliwa lakini hayakutumika.”

Dk. Bashiru amesema usimamizi mbovu katika mchakato wa kura za maoni, umesababisha wapiga kura wasiokuwa na sifa, kupiga kura na kusababisha malalamiko.

“Kuna malalamiko kwamba, usimamizi mbovu uliruhusu watu wasio na sifa, kupiga kura na kunyima haki wale wanaongombea. Kuna maeneo uwiano wa kijinsia haukufuatwa, mchujo haukuzingatia wakina mama,” amesema Dk. Bashiru.

Kufuatia changamoto hizo, Dk. Bashiru ameelekeza kamati za siasa za maeneo husika, kuzifanyia kazi dosari zilizojitokeza, ili kura za maoni za marudio zifanyike kwa haki.

“Kwa kuzingatia kanuni za CCM, katibu mkuu amepewa uwezo wa kutoa maelekezo zaidi ya uchaguzi, na kuagiza kamati ya siasa husika kuchukua hatua mbalimbali, nimewaiteni kufafanua maelekezo niliyotoa ili yatumike kusahihisha makosa yaliyojitokeza,” amesema Dk. Bashiru.

Aidha, Dk. Bashiru amewaonya wanachama wa CCM kutojihusisha na vitendo vya rushwa, katika zoezi la kura za maoni na uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Tusijihusishe na vitendo vya rushwa, tayari baadhi ya watu wako mikononi mwa TAKUKURU. Na mimi napenda kuhimiza kwamba TAKUKURU inakamata wala rushwa wakati wa uchaguzi, na baada ya uchaguzi. Wala rushwa ndani na nje ya CCM,” ameonya Dk. Bashiru.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!