Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Profesa Hoseah ajitosa sakata la Tanga Cement
Makala & UchambuziTangulizi

Profesa Hoseah ajitosa sakata la Tanga Cement

Ataka Serikali kutopinga maamuzi ya Mahakama barabarani

Spread the love

 

“HAKUNA namna ambayo serikali yaweza kukimbia maamuzi ya Mahakama kwa kutekeleza kile ambacho kimeamriwa kisimame; na au kinyume cha sheria. Pale ambapo Mahakama inazuia kutekelezwa kwa jambo fulani, ni sharti wahusika watekeleze maamuzi hayo. Anaandika Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

“Hii ni kwa sababu, utawala wa sheria hapa nchini umezungumzwa kwa uwanda mpana katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano na umeelezwa vizuri kwenye mashauri mbalimbali yaliyofunguliwa mahakamani. Utawala wa sheria unaashiria zaidi ya kutenda kwa mujibu wa sheria.

“Kwamba, utawala wa sheria, ni sharti uende mbali zaidi ya kufuatilia yaliyomo ndani ya sheria na kutizama ikiwa sheria husika zinaendana na misingi ya haki. Utawala wa sheria unapingana na utawala wa mkono wa chuma, na kwamba unaitaka serikali kuwa chini ya sheria na kufuata sheria zinazohusika. Pale ambapo kunakuwa na sheria zinazohalalisha uimla, basi hapo hakuna utawala wa sheria.”

Hivyo ndivyo anavyosema, Profesa Edward Hoseah, rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika na wakili wa Mahakama Kuu, kusisitiza dhana kuu ya serikali kuheshimu maamuzi ya Mahakama.

Profesa Hoseah, alikuwa akizungumzia kauli iliyotolewa bungeni na baadhi ya mawaziri, akiwamo Dk. Ashatu Kijaji, waziri wa uwekezaji, viwanda na biashara na Dk. Mwigulu Nchemba, waziri wa fedha na mipango, kwamba serikali inaendelea kusimamia muunganiko wa makampuni ya Twiga na Tanga Cement, wakati Mahakama imezuia mchakato huo.

Katika uamuzi wake wa 24 Machi mwaka huu, Baraza la Ushindani chini ya Jaji wa Mahakama Kuu, Salma Maghimbi; Wakili wa Mahakama Kuu, Onesmo Kyauke na Godwill Wanga, wameeleza kuwa uunganishaji wa makampuni hayo umezuiwa ili kulinda walaji.

Dk. Edward Hoseah

Aidha, Mahakama imesema, ikiwa uunganishaji huo utaendelea kufanyika wakati shauri linaendelea, basi mamlaka zinazohusika na usajili wa makampuni, uuuzaji wa hisa na wengine, wanazuiwa kuendelea na kazi ya kugawa hisa.

Kesi ilifunguliwa na Peter Hellar na kupewa namba 8 ya mwaka 2023, Kamishna wa Tume ya Ushindani; Scancem International DA, Fayaz Bhojani, William Erio na Hakan Gurdai.

Baraza la Ushindani wa Biashara (FCT), lilishawahi kutoa uamuzi wa kuzuia muunganiko wa kampuni hizo baada ya baadhi ya wadau – kampuni ya Saruji ya Chalinze, Chama cha Kutetea Haki za Watumiaji wa Bidhaa na Peter Heller – kuwasilisha malalamiko kupinga kuunganishwa kwa makampuni hayo.

Kwa mujibu wao, iwapo Twiga Cement itaruhusiwa kununua hisa za Tanga Cement, kuna uwezekano wa kuwapo na ukiritimba katika soko kwa kuwa Twiga Cement kupitia muungananiko huo, itakuwa na zaidi ya asilimia 68 katika soko.

Kwamba hilo likitokea, linaweza kusababisha upangaji wa bei, hivyo watumiaji wa bidhaa kushindwa kumudu gharama zake.

Muunganiko unaolalamikiwa, ni ule unaolenga kupitia kampuni ya Scancem International DA ambayo ni sehemu ya Heilderberg Cement inayomiliki Twiga Cement na Tanga Cement.

Lakini serikali kupitia kwa Waziri Dk. Kijaju inasema, imeamua imeamua kuendelea na mchakato huo, kwa kuwa mazingira ya awali kwa maana ya soko, yalikuwa yamebadilika na kwamba hakukua na zuio katika mchakato mpya bali ni ule wa kwanza.

Akisisitiza hoja yake, Profesa Hoseah anasema, “Mahakama ikishaamua jambo, liwe zuri au baya, linapaswa kuheshimiwa. Kutenda kinyume cha uamuzi wa Mahakama ni kuidharau mahakama. Katika hili la muunganiko wa Twiga na Tanga Cement, Mahakama imeshatoa maamuzi na hivyo, hakuna namna Serikali kutotekeleza maamuzi hayo.”

Anaongeza: “Kuhusu ulinzi wa walaji ambao ni muhimu kwa shauri lililoamriwa hivi karibuni na Baraza la Ushindani, walaji wanahitaji ulinzi dhidi ya hila hasa makubaliano/mikataba isiyo ya kishindani; matumizi mabaya ya utawala/ukuu kibiashara lakini pia muunganiko na ununuzi ambao lengo lake ni kuzuia/kuhodhi ushindani.’’

Profesa Hoseah anafanya marejeo ya mwanazuoni mwenzake, Profesa Nicholas Nditi na ripoti ya mkutano wa taifa wa wadau wa utawala wa sharia, uliyojadili “uimarishaji wa utawala wa sheria nchinia,’’ uliofanyika tarehe 10 – 11 Desemba 2015, jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia uhuru wa Mahakama, Profesa Hoseah anataja shauri la Hamisi Masisi na wenzake 6 dhidi ya Jamhuri, kufuatia Mkuu wa Mkoa wa Mara, kumuondolea dhamana iliyokuwa imetolewa na Hakimu Mkazi, Wilaya ya Musoma. Ni baada ya kuhisi hakuwa sahihi na haikuwa sahihi kwake kuamua hivyo.

Anasema, shauri hilo lilikatiwa rufaa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza. Baada ya usikilizaji wa shauri husika, Jaji Lameck Mfalila, aliweka wazi kuhusu umuhimu wa kuheshimu uhuru wa Mahakama.

Alisema, ‘‘…matendo ya mkuu wa mkoa dhidi ya warufani hawa ni bahati mbaya yameleta matokeo mengine ambayo yalipaswa kuachwa kwa muktadha wa uhuru wa Mahakama na sasa Mahakimu wa Mhakama ya Wilaya ya Musoma wamejikuta katika mtanziko na sintofahamu.

“Wameripoti kuwa wana woga wa kuamua mashauri yanayofanana na haya ambayo mengi yanakuja. Inaniumiza kufikiri kuwa katika hatua hii ya maisha ya taifa letu, kiongozi mmoja anaweza kufanya kwa namna ambayo inarudisha nyuma juhudi za utendaji bora wa Mahakama.

“Katika hatua hii, nina machache ya kufanya isipokuwa kuwaambia Mahakimu wa Musoma, kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kimahakama katika shauri hili na mashauri mengine, kwa mujibu wa viapo vyao, bila woga wala upendeleo.

“Lakini pia napenda kuionya Serikali ya Musoma kuwa itakuwa ni uvunjifu wa Katiba ya Nchi ambapo Mahakama hii italazimika kujilinda dhidi ya yeyote atakayetenda kinyume na kwa kuvunja Ibara zake. Moja ya jukumu la Mahakama hii ni kulinda Katibu ya nchi hii.’’

Anasema, hata tafakuri ya uhuru wa Mahakama imeelezwa vizuri nchini Ghana, moja ya nchi za jumuiya ya madola barani Afrika.

Ni moja ya shauri maarufu la Jamhuri dhidi ya Mahakama Kuu, Accra; ambapo Mahakama imeeleza kuwa ‘‘kutoheshimu amri ya Mahakama na kutoa sababu za kuhalalisha kutoheshimu kwa amri hizo, eti kwa kuwa amri hiyo isingepaswa kutolewa, hakuwezi kukubalika.”

Anasema, jambo sahihi la kufanya ni kuheshimu amri au kufungua shauri ili Mahakama iombwe amri hiyo iwekwe kando, na kwamba aliyeamua atapaswa kutoa sababu ya usahihi wa amri yake.

Anasema, kwa sababu za kisera ni muhimu kuwa mamlaka za mahakama na ukamilifu wa michakato yake uheshimiwe nyakati zote.

Kwa mujibu wa Profesa Hoseah, ni hatari sana kumpa mlalamikaji na wakili wake, haki ya kuamua ni amri zipi za Mahakama ni halali na wanastahili kuzitii na ikiwa hawafurahishwi nazo, basi hawapaswi kuzitii. Ni makossa amri ya mahakama yenye mamlaka juu ya jambo Fulani, kubadilishwa mtaani.

Profesa Hoseah ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) na pia Hakimu Mkazi Mkuu katika Mahakama ya Kisutu kutoka mwaka 1990 hadi 1995 anasema, “ni muhimu kutowawezesha mawakili katika ofisi zao kuwa wasimamizi wa mamlaka za Mahakama.

Gwiji huyo wa sheria nchini anasisitiza kuwa kuwafanya mawakili kama wasimamizi wa mamlaka za Mahakama, ni kuharibu kabisa usimamizi wa haki.

Akifafanua zaidi juu ya maamuzi ya Baraza la ushindani, Profesa Hoseah anasema, “kifungu cha 61 (2) cha Sheria ya Ushindani Na.8 ya mwaka 2002, inaeleza wazi kuwa uamuzi wa baraza kwenye rufaa chini ya kifungu hiki, utakuwa wa mwisho.”

Anaongeza, kifungu cha 84 (I) na (2) kinasema, “hukumu au amri ya Baraza kwenye jambo lolote mbele yake, itakuwa ya mwisho. Hukumu na amri za Baraza zitasimamiwa na kutekelezwa kama vile hukumu na amri za Mhakama Kuu zisimamiwavyo na kutekelezwa.”

Hivyo basi, Profesa Hoseah anasema, mtizamo wa utawala wa sheria upo wazi katika misingi inayohitaji kuwa Serikali lazima iwe chini ya sheria kuliko sheria kuwa chini ya serikali.

Walaji wa bidhaa na huduma wanaathiriwa sana na wanahitaji ulinzi dhidi ya hila kama vile mikataba isiyokidhi maslahi ya walaji na utawala usio wa haki kwenye soko; matumizi mabaya ya ukuu wa kibiashara na muunganiko na uuzaji ambao lengo lake ni kudhoofisha ushindani wa kibiashara.

Uhuru wa mabaraza yasimamiwayo na majaji na maafisa wengine wa Mahakama katika kutekeleza majukumu yao ya kimahakama yanatenda haya kwa mujibu wa sheria na matakwa ya Katiba, hivyo yeyote atakayevunja, atakuwa amedharau amri halali ya Mahakama.

Kwa maelezo yake, uamuzi wa baraza la ushindani na amri zake ni za mwisho. Wahusika wote wanapaswa kutii uamuzi au amri ama kufungua shauri mahakamani  kuomba kuwekwa kando sehemu ya uamuzi ambao hukubaliani nao.

Kuibuka watu, tena viongozi wa umma, kuamua kwenda kinyume na maelekezo ya Mahakama, katika nchi inayofuata utawala wa sheria, ni hatari kwa maslahi ya taifa na haileti taswira nzuri kwenye mfumo wa utawala wa sheria.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

error: Content is protected !!