CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema kitampima Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusu ustahimilivu wake katika masuala ya kisiasa, kwa kufanya mikutano ya hadhara. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hatua hiyo imetangazwa leo Jumanne, tarehe 27 Aprili 2021, na Mwenyekiti wa CUF, Prof, Ibrahim Lipumba, wakati akichambua hotuba ya Rais Samia aliyoitoa bungeni jijini Dodoma, tarehe 22 Aprili mwaka huu.
Katika hotuba hiyo, Rais Samia alisema muelekeo wa serikali yake ya awamu ya sita, ni kudumisha mazuri ya uongozi wa awamu zilizopita, kuendeleza mema yaliyopo pamoja na kuleta mengine mapya.
“Naamini kama chama tutaweza kupata fursa ya kueneza sera zetu za haki sawa na furaha kwa wote kwenye majukwaa ya siasa.
“Namna ya kuweza kumpima kama kweli atatembea kwenye maneno yake, ni sisi kutumia fursa hii kuweza kujipanga kikamilifu na kuweza kueleza sera zetu kwenye umma wa Watanzania,” amesema Prof. Lipumba.
Katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, vyama vya siasa vilipigwa marufuku kufanya mikutano ya hadhara, isipokuwa kwa wabunge ambao waliruhusiwa kufanya mikutano hiyo katika majimbo yao.
Akichambua hotuba ya Rais Samia, Prof. Lipumba amesema “nimetiwa moyo na kauli yake kwamba, muelekeo wa serikali yake ni kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya.
“Tafsiri ya muelekeo huu kwa upande wangu, inatafsiri kwamba mabaya yaliyokuwa yanatokea siku za nyuma yataachwa, hakuainisha mabaya hayo lakini kusema tuyaendeleze yale mazuri, inatoa fusra kwa yale yaliyokuwa mabaya yaweze kuwekwa kando.”

Mwenyekiti huyo wa CUF amesema, hotuba hiyo imemtia moyo, kwani Rais Samia alifungua milango kwa wabunge kuikosoa Serikali yake, sambamba na kuruhusu wananchi kuipa ushauri.
“Katika hotuba yake, alivyoyaeleza yanaleta matumaini ya kuwepo serikali sikivu ya kuweka sera zinazotekelezeka.
“…, pia kuna mambo machache mapya muhimu kwa taifa letu aliweka hadharani, amewakaribisha wabunge wasimamie na kuikosoa serikali kiustarabu na wananchi wamepewa fursa ya kuishuri,” amesema Prof. Lipumba.
Leave a comment