Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Prof. Lipumba apata pigo jingine
Habari za Siasa

Prof. Lipumba apata pigo jingine

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF)
Spread the love

MAHAKAMA ya Rufaa nchini imetupilia mbali pingamizi lililowekwa na wafuasi wa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), anayetambuliwa na msajili wa vyama vya siasa, Prof. Ibrahimu Lipumba. Anaripoti Faki Sosi.… (endelea).

Pingamizi lililotupwa msingi wake mkuu, ni shauri Na. 75 ya mwaka 2017,lililofunguliwa mahakama kuu, kanda ya Dar es Salaam na bodi ya wadhamini halali ya CUF.

Katika shauri hilo, bodi ya wadhamini ya CUF, inahoji mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kumrejesha Prof. Ibrahim Lipumba, kwenye nafasi yake ya mwenyekiti.

Aidha, wakati shauri liko katika hatua za usikilizaji, bodi iliwasilisha mahakamani maombi ya kumtaka Jaji Sekieti Kihiyo, kujiweka kando na shauri lililokuwa mbele yake. Jaji Kihiyo aliridhia ombi hilo.

Hata hivyo, wafuasi wa Lipumba, walipinga maamuzi hayo. Wakawasilisha rufaa mahakama ya rufaa.

Katika maombi yao Na. 43/01/2017 mbele ya mahakama ya rufaa, wafuasi wa Prof. Lipumba waliitaka mahakama kuamuru shauri hilo liendelee kusikilizwa na Jaji Kihiyo.

Walidai kuwa utaratibu wa kuwasilisha maombi ya kumtaka jaji huyo kujiondoa yaliyowasilishwa na upande wa walalamikaji – bodi ya wadhamini – haukufuata taratibu.

Baraza la Wadhamini la CUF linamtuhumu Jaji Mutungi, kukivuruga chama hicho; kuingilia utendaji wake na kuvunja katiba yake.

Baraza la wadhamini la CUF linaongozwa na Abdallah Said Katau (mwenyekiti) na Joran Bashange (katibu).

Madai hayo yanafuatia hatua ya msajili huyo kumrejesha Prof. Lipumba kwenye uenyekiti wa chama hicho, kinyume na kanuni, Katiba na maamuzi halali ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT).

CUF kimekumbwa na mgogoro kufuatia hatua ya Jaji Mutungi, kuamua kinyume na sheria ya vyama vya siasa, kumtangaza Prof. Lipumba, kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho.

Kufuatia uamuzi huo, baraza likawasilisha Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, maombi yaliyoruhusu kufunguliwa shauri dhidi ya Jaji Mutungi; Prof. Lipumba na watu wengine 12 waliosimamishwa uanachama.

Shauri dhidi ya Jaji Mutungi, Prof. Lipumba na wafuasi wao wengine, hivi sasa, linasikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Wilfred Dynsobera.

Pamoja na mengine, baraza linamtuhumu Jaji Mutungi, kujihusisha na masuala ya ndani ya CUF, kinyume na sheria ya vyama vya siasa na kanuni zake. Linamtuhumu kumbeba Prof. Lipumba na kusaidia uasi ndani ya chama.

Akisoma uamuzi wake mahakamani leo Ijumaa, Jaji Musa Kipenka amesema, kesi hiyo itaendelea kusikilizwa na Jaji Dynsobera kwa kuwa taratibu zote za kujiondoa kwa Jaji Kihiyo zilifuata msingi mkuu wa kisheria.

Jaji Mutungi anatuhumiwa na bodi kuingilia maamuzi halali ya chama hicho yaliyobariki kujiuzulu kwa Prof. Lipumba kwenye wadhifa wake.

Prof. Lipumba alitanganza kujiuzulu kwa hiari uenyekiti wa CUF kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa 25 Oktoba 2015.

Maamuzi yake yalibarikiwa na mkutano mkuu wa taifa wa chama hicho uliofanyika kwenye hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza, tarehe 21 Agosti 2017.

Katika barua yake ya kujiuzulu, Prof. Lipumba alimjulisha Maalim Seif Shariff Hamad – katibu wa mamlaka iliyomchangua kuwa mwenyekiti – uamuzi ambao tayari alishachukua na kuutekeleza.

Kabla ya kuwasilisha barua yake kwa Malim Seif, watu wa aina mbalimbali na rika tofauti, walimuomba abadilishe uamuzi wake wa kujiuzulu. Alikataa. Alisema, “sitarudi nyuma. Nafsi imenisuta. Nang’atuka.”

Akaongeza, “najua kuwa uamuzi wangu utawaumiza wengi, lakini CUF ni taasisi. Nitatoa ushirikiano nitakapohitajika. Nitabaki kuwa mwanachama wa kawaida.” Akatoka ofisini. Akaacha kufanya shughuli za chama.

Mapema wiki hii, Mahakama Kuu iliipiga marufuku bodi ya wakurugenzi iliyoundwa na Prof. Lipumba kujihusisha na shuhguli zozote za chama hicho.

Katika shauri hilo, bodi ya wadhamini halali ya CUF inawakilishwa na mawakili, Halfani Daimu, Juma Nassoro na Hashimu Mziray.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!