Tuesday , 18 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CCM ‘yachotewa’ na serikali Sh. 1.7 bilioni
Habari za SiasaTangulizi

CCM ‘yachotewa’ na serikali Sh. 1.7 bilioni

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
Spread the love

MFUKO Mkuu wa Serikali (HAZINA), umetikishwa baada ya kuchotwa mabilioni ya shilingi na kuelekezwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Hamisi Mguta … (endelea).

Mabilioni hayo ya shilingi za umma yamechotwa kutoka hazina na kupelekwa CCM, kwa maelezo kuwa ni “deni la serikali kwa chama hicho.”

Taarifa kutoka wizara ya fedha, Ikulu na ofisi kuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam zinasema, fedha hizo zimetolewa kwenye mapato ya Desemba mwaka huu.

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja siku tatu baada ya CCM kumaliza mkutano wake mkuu wa 19 mjini Dodoma.

Mbali na mkutano huo mkuu, chama hicho tawala kilifanya mikutano ya jumuiya zake tatu – wanawake (UWT), vijana (UV-CCM) na wazazi.

Mikutano mikuu ya jumuiya za CCM, pamoja na mkutano mkuu wa chama chenyewe, inaelezwa kuwa unakadiwa kutumia zaidi ya Sh. 4 bilioni bila kujulikana wazi chanzo chake.

Aidha, kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja kipindi ambacho katibu mkuu wa chama hicho, Abdulrahaman Kinana, amenukuliwa kuwaeleza wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kuwa chama chake hakikuwa na fedha ya kuendesha mikutano yake. 

Kinana alisema, wakati wa kuelekea kufanyika mikutano hiyo, alilazimika kumuona mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli, ili kumjulisha juu ya ukatana unaokikabili chama chake.

Kwa mujibu wa waraka wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango ambao MwanaHALISI Online umeuona, serikali imekilipa chama hicho kiasi cha Sh. 1.7 bilioni ili kufidia kile ilichoita, “shule yake iliyotaifisha.”

Inayotajwa kuwa shule ya CCM ambayo imetaifishwa na serikali na hivyo kujaribu kuhalalisha malipo hayo, imetajwa kwa jina la “Shule ya Sekondari Omumwani” iliyopo mjini Bukoba, mkoani Kagera.

Dk. Mpango anaeleza katika waraka wake huo, “kiasi cha Sh. 1,772,000,000 kinalipwa kwa ajili ya kulipia fidia kwa Jumuiya ya Wazazi wa CCM kutokana na Shule ya Sekondari Omumwani iliyopo Bukoba kutwaliwa na Serikali.”

Wakati serikali inajikamua kulipa deni hilo, maelfu ya wakandarasi wa ndani wanadai mabilioni ya shilingi na wengine wako mbioni kufunga ofisi zao kutokana na kushindwa ukata.

MwanaHALISI Online limeelezwa na vyanzo vyake vya taarifa kuwa serikali haikufuata taratibu zozote za sheria ya manunuzi ya umma (PPRA) ya mwaka 2004 wakati wa ununuzi wa wa shule hiyo.

Wala serikali haikuwahi kufanya tathimini iliyo huru na yakinifu ya thamani halisi ya majengo ya shule iliyolipwa fidia; ardhi na mali zingine zilizopo kwenye shule hiyo.

Tangu kumalizika uchaguzi mkuu uliyopita, mapato ya CCM yamepungua kutokana na kupukutishwa kwa ruzuku yake kulikotokana na kufanya vibaya kwenye uchaguzi mkuu uliyopita. 

Kabla ya uchaguzi mkuu uliyopita, CCM kilikuwa kinapata kwenye mgawo wake wa ruzuku kutoka serikali kiasi cha Sh. 1.2 bilioni, kila mwezi. Sasa kinapata chini ya Sh. 900 milioni.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mazingira magumu ya JPM yamechangia ‘Comedy Journalism’

Spread the loveMwenyekiti wa Kamati ya kufuatilia hali ya uchumi wa vyombo...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

RC Chalamila: Nimeacha ubabe

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chamalila amemthibishia...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia atoa ujumbe mzito Sikukuu Eid Al Adha

Spread the loveKATIKA kusherehekea Sikukuu ya Eid Al Adha, Rais wa Tanzania,...

BiasharaHabari za Siasa

Dk. Biteko aipongeza NMB kwa kuanzisha utoaji wa bima ya mifugo

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!