May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Kabudi: Elimu ya sheria kutolewa nchini

Prof. Palamaganda Kabudi, Waziri wa katiba na Sheria

Spread the love
PROFESA Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria amesema, serikali ina mpango wa kutoa elimu ya sheria kwa makundi yote ya kijamii ili kutokomeza ukatili. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Prof. Kabudi katoa maelezo hayo baada ya swali la Wanu Hafidh Ameir (Mbunge Viti Maalum) kuuliza, kwamba serikali ina mpango gani wa kuhakikisha elimu ya sheria zinazowapa kinga na haki wanawake, inatolewa kwa wanawake wote mjini na vijijini?

Waziri huyo amesema, mkakati huu unalenga kuimarisha na kulinda haki za wanawake na watoto, kuanzisha madawati ya msaada wa kisheria katika vituo vya polisi na magereza, kutafsiri sheria zote kwa lugha ya Kiswahili na kuendelea kutoa mafunzo ya sheria kwa wananchi kupitia mikutano na mihadhara.

“Mwaka 2017 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sheria Na.1 ya Mwaka 2017. Madhumuni ya sheria hii pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha msaada wa kisheria, ambao una maana ya utoaji wa elimu na ushauri wa kisheria; uandishi wa nyaraka za kisheria/kimahakama; na au uwakilishi mahakamani kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili; unatolewa.

“Tangu kutungwa kwa sheria hiyo hadi Machi 2021, takribani wanawake 3,162,421 mijini na vijijini, wamepatiwa msaada wa kisheria kupitia madhimisho ya wiki ya sheria, wiki ya msaada wa kisheria ambayo inaadhimishwa kila mwaka katika mikoa yote hapa nchini, vipindi vya redio na luninga.

“Pia ziara za viongozi na wataalamu wa wizara katika magereza na mahabusi za polisi na majukwaa mbalimbali. Lengo la serikali ni kutimiza azma ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki kwa gharama nafuu na kwa wakati,” amesema.
error: Content is protected !!