PROFESA Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria, amewataka Watanzania kutoingilia kati sakata la Masheikh 23 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar, kwa kuwa liko mahakamani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Waziri huyo wa Katiba na Sheria ametoa kauli hiyo leo Jumatano tarehe 28 Aprili 2021, bungeni jijini Dodoma.
Akizungumzia sakata hilo, Prof. Kabudi amesema, ushahidi wa kesi ya jinai Na. 121/2021 inayowakabili Masheikh hao katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, umekamilika, hivyo wananchi wanapaswa kusubiri uamuzi wa mahakama.
“Sasa ushahidi umekamilika, kesi iko mahakama kuu. Tuiachie mahakama kuu itoe uamuzi wake na asiyeridhika na maamuzi yatakayotolewa na mahakama, akate rufaa katika Mahakama ya Rufani ambayo ni ya muungano,” amesema Prof. Kabudi.
Prof. Kabudi amesema, kesi hiyo ilihamishiwa kutoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, baada ya upelelezi wake kukamilika.
“Shauri ambalo liko mahakamani na linaendelea ni shauri la masheikh wa uamsho, mnamo tarehe 15 Septemba 2020, shauri la jinai 21/2014 lililokuwepo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lilifunguliwa rasmi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, mara baada ya upelelezi kukamilika,” amesema Prof. Kabudi.
Prof. Kabudi amesema, usikilizwaji wa kesi hiyo ulipaswa kuanza tarehe 25 Machi 2021, ulikwama kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, kilichotokea tarehe 17 Machi mwaka huu, kwenye Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam.
“Tarehe 17 Septemba 2020 mchakato wa kuhamisha kesi husika katika mahakama kuu ulikamilika, kesi hiyo ilikuwa ianze kusikilizwa tarehe 25 Machi 2021, lakini kutokana na msiba uliotupata ilisogezwa mbele hadi mwanzoni mwa mwezi Aprili, kwa sasa mahakama kuu imeanza kusikiliza kesi hiyo 121/2021 kuanzia tarehe 12 Aprili 2021.”

Masheikh hao waliakamtwa mwaka 2012 kisiwani Unguja, Zanzibar, kwa tuhuma za kuchochea vurugu.
Kauli hiyo ya Prof. Kabudi imetolewa baada ya mjadala wa sakata hilo kuibuka bungeni hivi karibuni, ambapo baadhi ya wabunge walihoji kwa nini mwenendo wa kesi hiyo unasua sua.
Miongoni mwa wabunge waliohoji hayo, ni Mbunge wa Kawe (CCM),Askofu Josephat Gwajima na Mbunge wa Chonga, Salum Mohammed Shafi.
Akichangia katika mjadala wa Mkadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Shafi alihoji kwa nini kesi hiyo haikusikilizwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, badala ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Baada ya kuhoji hayo, Prof. Kabudi alijibu “hakuna mahakama yoyote inayoinyang’anya mahakama nyingine kesi sababu mahakama sio ambulance haifuati mgonjwa bali inapelekewa kesi, kwa hiyo kama kuna kesi inayohusu raia wa Tanzania Zanzibar katika Mahakama Kuu ya Tanzania, yupo aliyeipeleka.”
SE muku