Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Nyundo 10 za Askofu Bagonza ‘Spika wetu Vs Spika wao’
Habari za Siasa

Nyundo 10 za Askofu Bagonza ‘Spika wetu Vs Spika wao’

Askofu Benson Kagonza, KKKT Dayosisi ya Karagwe
Spread the love

 

CHAMA tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo Alhamisi, tarehe 20 Januari 2022, kitatoa dira ya nani atakuwa Spika wa Bunge la nchi hiyo kurithi nafasi iliyoachwa wazi na Job Ndugai aliyejizulu hivi karibuni. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan ataongoza kikao cha kamati kuu kitakachofanyika makao makuu ya chama hicho, ‘White House’ jijini Dodoma ambapo kitakuwa na jukumu la kuchakata majina 70 ya waliojitosa kuwania nafasi hiyo.

Mara baada ya kuteua majina matatu miongoni mwa hao 70, watakwenda kupigiwa kura na kamati ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kumpata mmoja atakayekwenda kushindanishwa na wagombea wa vyama vingine bungeni.

Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa CCM

Uchaguzi wa spika wa Bunge, utafanyika tarehe 1 Februari 2022, siku ya kwanza ya mkutano wa sita wa Bunge jijini Dodoma.

Asubuhi ya leo Alhamisi, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Dk. Benson Bagonza ameuzungumzia mchakato huo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuibua maswali kumi.

Maswali hayo yaliyoanza na kichwa cha habari “Spika wetu Vs Spika wao” haya hapa;

1. Upo mgawanyiko ndani ya bunge juu ya ama Spika ajaye awe ni Mbunge au asiwe ni Mbunge. CCM wasilipuuze hili.

2. Zipo kambi tatu kubwa na zote zina wagombea (JPM, JK na SSH). Wenye kambi hawana habari lakini wafuasi wao wapo. Msiogope, Uchaguzi usio na makundi haunogi.

3. Kuna wagombea wachache sana wasio na kundi na wanafaa kwa nafasi hii lakini hawana wafuasi.

4. Suala la umri wa Spika linabishaniwa. Tumesahau kuwa baraza la kwanza la mawaziri wa Tanganyika huru lilikuwa na umri wa kuanzia miaka 31 hadi 39.

5. Mijadala kuhusu mchakato wa kumpata Spika ajaye imetawaliwa na majina kuliko masuala mazito yanayoikabili nchi. Kujadili majina kutatupatia Spika wao ambaye ni mtumwa wa wabunge na mateka wa serikali. Kujadili masuala kutatupatia Spika wetu. Hata wabunge hawatalitamani bunge linaloongozwa na Spika wao.

6. Kuna wabunge wengi hawakushinda kura za maoni. “Nasikia” kuna wabunge wengi walinunua ushindi wa kura za maoni. “Nasikia” kuna wabunge wengi hawakushinda Uchaguzi. Mchakato huu unaibua mengi. Makundi haya matatu yanataka Spika wao. Wananchi tunataka Spika wetu. CCM ina dhamana ya kutupatia Spika wetu siyo Spika wao.

7. Madai ya Katiba Mpya yanachukua sura mpya kila siku. Hoja za kuzuia ni nyepesi kuliko zinazodai katiba mpya. Madai yasipoongozwa, yataongoza. Mwenye njaa anayebisha hodi asipofunguliwa mlango, aliye ndani hatalala usingizi. Mfungulie ale alale.

8. Wapo wanaodai katiba mpya yote. Wapo wanaodai mkono, masikio na mdomo wa katiba. “Nimesikia” serikali iko tayari kukubali mguu na ulimi wa katiba mpya. Mtoto asiye na miguu na ulimi ni mzigo kwa mzazi kuliko alivyo mzigo kwa binti wa kazi. Kubalini katiba yote, ni akiba uzeeni. Kama mnabisha, kaulizeni huko Kongwa.

9. Kwenye Uchaguzi wa Spika bungeni kuna vita baridi kati ya UKWELI na UHALALI. Mjadala wa sasa ni juu ya kinachoitwa Covid 19. CCM ina dhamana ya kutatua hili na kujijengea heshima. Siyo kila kweli ni halali. Bungeni ni mahali patakatifu. Spika wetu awe msafi kupitia kura halali TU.

10. Kuna wakati ukiwagawa unawatawala kirahisi. Zipo nyakati ambazo ukiwagawa hawatawaliki tena. Lakini zipo nyakati ambazo ukiwagawa nao wanakugawa. Hili la tatu ni baya sana. La pili ni baya na hatari. La kwanza limezoeleka na kumbwetesha mtumiaji. Kama mwenye nyumba angejua mwizi anakuja saa ngapi, angekesha.

Nimewachosha kwa kuandika mengi? Machache yana umbeya mwingi.

Twende kulipa ada za shule. Ada za uanachama wa vyama zisubiri.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!