November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nyalandu, Lema, Mch. Msigwa watoa neno Lissu kuvuliwa ubunge

Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema

Spread the love

HATUA ya Job Ndugai, Spika wa Bunge kumvua Tundu Lissu Ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki kwa kile alichoeleza kwamba hajatoa taarifa ya kutohudhuria vikao vya bunge kwa zaidi mwaka mmoja, imewaibua wanasiasa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Baadhi ya wanasiasa wameibuka na kueleza maoni yao kuhusu hatua hiyo, huku wengi wao wakionesha kushangazwa na sababu zilizopelekea Lissu kuvuliwa ubunge, ikiwemo madai ya kutotoa taarifa kwa Spika kwa muda wote ambao hakuhudhuria katika vikao vya bunge.

Lazaro Nyalandu, aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini amesema hatua ya Spika kumvua ubunge Lissu huku akiwa nje anapatiwa matibabu  ya majeraha aliyopata baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana, ni aibu na fedheha kwa demokrasia.

“Kitendo cha Mh. Spika kumvua Ubunge Mh. @tundulisu, huku akiwa anaendelea na matibabu Ubelgiji kufuatia shambulio dhidi yake la kupigwa risasi, ni aibu na fedheha kwa demokrasia. Tundu Lissu ameonewa sana, haipendezi kuendelea kumuumiza zaidi. Hakika haki huinua Taifa. #BungeTZ,” ameandika Nyalandu katika ukurasa wake wa Twitter.

Mch. Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika kuwa, hatua hiyo si ya kibinadamu na wala haina tija kwa taifa.

“Hatua ya kuufuta ubunge Wa Tundu Lissu, ni kuuonyesha ulimwengu jinsi ambavyo hatuna tena ubinadamu! Na jambo hili halina tija kwa serikali ya awamu ya tano wala kwa CCM YENYEWE! This is a downfall to the ruling party!” ameandika Mch. Msigwa.

Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini amesema moyo wake unavuja damu kutokana na hatua ya Spika Ndugai kumvua ubunge Lissu.

“Mh. Spika umemvua Mh. Tundu Lissu Ubunge? Moyo wangu unavuja damu….Mungu nisaidie,” ameandika Lema.

Spika Ndugai wakati akihitimisha kikao cha 55 cha mkutano wa  15 jana tarehe 28 Juni 2019 bungeni jijini Dodoma, alisema jimbo la Singida Mashariki lililokuwa linashikiliwa na Lissu lipo wazi, na kwamba amemjulisha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili aendelee na taratibu za kulijaza.

Spika Ndugai amesema Lissu ameshindwa kumpa taarifa katrika kipindi ambacho hakuhudhuria vikao vya bunge, pamoja na kutowasilisha tamko la mali zake na kwamba vitendo hivyo vimevunja sheria ya uchaguzi.

error: Content is protected !!