Wednesday , 8 May 2024
Home Habari Mchanganyiko NMB yafuturisha Dar, Mufti Zubery atoa neno
Habari Mchanganyiko

NMB yafuturisha Dar, Mufti Zubery atoa neno

Spread the love

 

BENKI ya NMB nchini Tanzania, imefuturisha waumini wa Kiislamu jijini Dar es Salaam huku ikiwakumbusha kuutumia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kufanya tafakari juu ya maadili yanayounganisha jamii, upendo kwa familia zao, shukrani kwa Mungu, kufanya toba za dhati na ushiriki endelevu wa ibada hata baada ya mfungo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa jioni ya jana Alhamisi, tarehe 14 Aprili 2022 na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na waumini hao, viongozi wa dini, Serikali na wageni waalikwa.

Pia, Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakary Zubery Ally ndiye alikuwa mgeni rasmi.

Mponzi alisema: “katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani, ni wakati sahihi kwa Waislamu na jamii kwa ujumla kutafakari juu ya maadili yanayotuunganisha binaadamu wote, upendo kwa familia zetu, shukrani kwa Mungu, kufanya toba za dhati na ushiriki endelevu wa ibada.”

“Kwa hiyo huu ni mwezi muhimu kwa Waislamu na kwa jamii kwa ujumla, nasi NMB tunakitumia kipindi hiki kujumuika na wateja wetu, kwa sababu tunaamini katika mwezi huu, jamii zetu hustawishwa kwa swala na toba za dhati zinazotolewa wakati huu,” alisema.

Mponzi alisema Mwezi wa Ramadhani ni baraka kwa maisha ya watu wengi na taifa kwa ujumla huku akimshukuru Sheikh Mkuu, viongozi wa dini na Serikali, wateja na wafanyakazi wa benki hiyo kwa kutumia muda wao kujumuika katika hafla hiyo, ambayo haikufanyika miaka miwili kutokana na mkwamo wa Uviko 19.

“Nawatakia Ramadhani njema na mkawe na mwisho mwema wa mfungo, NMB tunatoa wito kwenu kwamba baada ya mfungo, ibada na wema uendelee, kwani kwa kufanya hivyo tutaendelea kupata thawabu na kujenga jamii yenye upendo na amani,” alisema Mponzi aliyemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu, Ruth Zaipuna.

Kwa upande wake, Mufti Aboubakary Zubery aliushukuru uongozi wa NMB na kuupongeza kwa kile alichokiita ‘Moyo wa Kuthamini na Kujali,’ uliowafanya waone umuhimu wa kukutanisha Waumini wa Kiislamu na kuwafanyia moja kati ya Furaha Mbili za Mfungaji wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani zilizotajwana Mtume Muhammad (S.A.W)

“Mtume Muhammad (S.A.W) amesema: Mwenye Kufunga Ramadhani huwa na nyakati mbili za furaha. Furaha ya kwanza ni pale anapohitimisha funga ya siku wakati wa kufuturu jioni na furaha ya pili ni wakati wa kuingia kwake peponi kutokana na kukubaliwa kwa ibada hiyo.

“Sasa hii furaha ya kwanza ambayo nyinyi mmeijaalia hadi sisi kukutanishwa hapa, mnastahiki kupongezwa na mnastahili kuonwa kuwa mna tabia nzuri. Viongozi wa NMB mmeonesha tabia njema ya ‘Kuthamini na Kujali, Mungu awabariki,” alisema.

“Msingekuwa na moyo wa kuthamini na kujali, msingeona umuhimu wa kukusanya watu kuwafuturisha. Futari hii ina maana kubwa sana, inajenga undugu, inakutanisha watu waliopotezana, pia inaondoa mafundo nyoyoni mwa walioalikwa, lakini pia watu wanafurahi kwa kule kufuturishwa.

“Dua njema mnazoombewa na waumini na waalikwa waliohudhuria hapa, zitaenda kuwa baraka, heri na chachu ya mafanikio ya viongozi wa benki hii na taasisi yenu kwa ujumla. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awanyanyue zaidi muendelee kufanya yaliyo mema kwa jamii,” alimaliza Mufti Zubeir.

Naye Meneja wa NMB, Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, aliwashukuru waumini wa Kiislamu, viongozi wa dini, serikali na wageni waalikwa waliohudhuria hafla hiyo, kwani wangeweza kwenda kupata futari kwingine, hasa majumbani, lakini wakatumia muda ambao ni rasirimali muhimu, kuungana na NMB.

“Hakika ninyi ni marafiki wa kweli wa NMB, utamaduni huu ulikuwepo, ukasimama kwa muda na sasa umerejea tena, hii sio mara ya mwisho, tutakapowaita tena, msisite kuungana nasi. Wito kwa Watanzania ni kujiunga na benki hii, huku tukiwaomba wote mliohudhuria hapa kuwa mabalozi wema wa NMB kwa jamii,” alisema Donatus.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoMichezo

Kengold wakabidhiwa kombe NBC Championship

Spread the loveMdhamini mkuu wa Ligi Daraja la Kwanza (NBC Championship) Benki...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC, SILABU waungana kufikisha elimu ya fedha majumbani

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano...

AfyaHabari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kisukari cha mimba ni nini?

Spread the loveKisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi...

error: Content is protected !!