May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NCCR-Mageuzi yakubali kushiriki mkutano TCD na Rais

Edward Sembeye, Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma wa NCCR Mageuzi

Spread the love

 

CHAMA cha NCCR-Mageuzi, kimetengua azimio lake la kutoshiriki mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya mapendekezo yake kufanyiwa kazi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, tarehe 11 Machi 2022, jijini Dar es Salaam, na Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma Taifa, Edward Simbeye, akitangaza maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho, iliyoketi jana jijini humo.

“Kamati kuu imezingatia mambo hayo na imejiridhisha hoja zote kinzani tulizotoa zimezingatiwa na kwa msingi huo hatutakuwa na sababu yoyote ya kutoshiriki mkutano wa majadiliano ya amani kule Dodoma tarehe 30 na 31, Machi 2022,” amesema Simbeye.

Simbeye amesema, “Kamati Kuu imekubali kutengua azimio lake la kutoshiriki na sisi NCCR-Mageuzi tutashiriki kama wanachama halali wa TCD, lakini mambo tuliyokubaliana yametekelezwa pasi na shaka. Hivyo tutashiriki.”

Mkuu huyo wa Uenezi NCCR-Mageuzi, ametaja miongoni mwa mapendekezo yao yaliyofanyiwa kazi, ikiwemo ya Rais Samia kukubali kufanya mkutano wa awali na wadau wa vyama vya siasa kabla ya mkutano huo.

Simbeye amesema, Rais Samia atafanya mkutano na viongozi wa vyama vya siasa tarehe 18 Machi mwaka huu, ambapo NCCR-Mageuzi itawakilishwa na Mwenyekiti wake, James Mbatia.

“Tulisema ili tushiriki tukiwa na amani kuwe na mkutano mdogo wa vyama vya siasa vinavyounda TCD pamoja na Rais, tunaamini katika kweli, tuzungumze, tutibiane makovu ya uchaguzi, tuzungumze uso kwa uso kabla ya kwenda kwa umma,” amesema Simbeye.

NCCR-Mageuzi, kilikataa kushiriki mkutano wa wadau wa vyama vya siasa ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, na kufanyika Desemba 2021 jijini Dodoma, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Samia.

Chama hicho kiligoma kushiriki mkutano huo kikitaka maridhiano juu ya changamoto zilizojitokeza kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Simbeye amesema, NCCR-Mageuzi kinahitaji muafaka wa kitaifa na Tanzania iliyo salama na yenye amani

“Tunataka kila mtu apate haki yake, ndiyo maana tulikuwa tunasimamia haki. Pale ambapo kuna haki tunasimamia haki, pale ambapo hakuna haki hatutakuwa wavivu kusema hapa hakuna haki na tutatoa njia ya kupata haki,” amesema Simbeye na kuongeza:

“Ndiyo maana tumekubaliana kwamba kuna mwanga wa kushirki mkutano huu na baada ya hapo majadiliano mengine yataendelea.”

error: Content is protected !!