Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mwandishi Kabendera, afunguliwa kesi ya kushirikiana na wahalifu
Habari za SiasaTangulizi

Mwandishi Kabendera, afunguliwa kesi ya kushirikiana na wahalifu

Mwandishi wa habari Erick Kabendera alipofikishwa mahamakani Kisutu leo
Spread the love

MWANDISHI wa habari za uchunguzi nchini, Erick Kabendera, hatimaye amefikishwa mahakamani kwa makosa matatu, likiwamo utakatishaji fedha na kushirikiana na kinachoitwa, “makundi ya kihalifu.” Anaripoti Faki Sosi … (endelea). 

Kabendera aliyekamatwa na maofisa wa vyombo vya usalama vya Tanzania, nyumbani kwake, Mbweni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, ameshitakiwa pia kwa makosa ya ukwepaji kodi na utakatishaji fedha.

Mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, Augustine Rwizile, Wakili wa Serikili Mkuu Faraja Nchimbi, kwa niaba ya wenzake wawili, Paul Kadushi na Simon Wankyo, ameeleza mahakama kuwa Kabendera alitenda makosa hayo kati ya mwaka 2015 na Agosti mwaka huu.

Katika shitaka la kwanza, Nchimbi amedai kuwa mwandishi huyo wa habari, mtafiti wa masuala ya kisiasa na kiuchumi na usalama wa kikanda, anadaiwa kujihusisha na mtandao wa uhalifu. Kosa hilo ni kinyume na kifungu kidogo cha 4(1)(c) cha jedwari la kwanza na kifungu cha 56(1) na 60(2) cha makosa ya uhujumu uchumi.

Kumeelezwa mahakamani hapo, kwamba kati ya Januari 2015 na Julai 2019, kwenye mkoa wa Dar es Salaam, pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, mshitakiwa alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Katika shitaka la pili, Kabendera anatuhumiwa kukwepa kulipa kodi. Kosa hilo anadaiwa kulitenda kati ya Januari 2015 na Julai 2019, katika maeneo tofauti mkoani Dar es Salaam.

Upande wa Jamhuri umeeleza kuwa Kabendera amekwepa kodi ya Sh. 173,247,047.02 kinyume na kifungu namba 105(A) cha sheria ya kodi ya mapato.

Amedai, “bila kuwa na sababu za msingi ya kisheria, mshtakiwa alishindwa kulipa kodi ya kiasi cha Sh. 173.2 milioni kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).”

Shitaka la tatu limetajwa mahakamani hapo kuwa ni utakatishaji fedha, Kabendera anadaiwa kuwa kinyume na kifungu cha 3(u), 12(d) na 13(a) cha sheria ya utakatishaji fedha, katika tarehe tofauti Januari 2015 na Julai 2019, ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, mshitakiwa alijipatia fedha kiasi cha Sh.173 milioni huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa tangulizi ambayo ni kukwepa kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.

Baada ya kusomewa mashataka hayo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu chochote kwa kuwa kesi hiyo ni ya uhujumu uchumi na mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza.

Hata hivyo, upande wa mashtaka umedai, upelelezi wa kesi hiyo upo mbioni kukamilika, huku upande wa utetezi ukaomba upelelezi huo uharakishwe ili waweze kuendelea na hatua nyingine.

Katika hatua nyingine wakili wa upande utetezi Jebra Kambole, waliomba mahakama kuondoa maombi yao ya awali ya kutaka mshitakiwa afikishwe mahakamani na kupatiwa dhamana kwa sababu, mashtaka yanayomkabili hayana dhamana.

Hakimu Rwizile aliondoa maombi hayo kama walivyoomba upande wa utetezi; na kuiahirisha kesi hiyo hadi tarehe 19 Agosti 2019.

Mapitio ya MwanaHALISI ONLINE, yamebaini upungufu katika hati ya mashitaka. Kwa mfano, katika kosa la pili linalohusu ukwepaji wa kodi, kwa mujibu wa taratibu, kodi inalipwa kutokana na kiasi unachopata; na si fedha yote unayopata.

Ukiangalia kiasi kinachotajwa kuwa hakikulipwa kodi kwenye kosa la pili, ni kiasi kilekile anachodaiwa kukipokea.

Kwa maneno mengine, hakuna sheria inayokutaka kulipa kodi fedha yote uliyonayo. Kodi hulipwa kutoka kwenye kiasi ulicholipwa kwa mujibu wa viwango vilivyoanishwa na sheria. Kiwango cha juu kabisa nchini, ni asilimia 30 ya mapato.

Kabla ya uamuzi wa kumfikisha mahakamani leo, Kabendera alikuwa tayari amekaa lupango ya kituo cha Polisi Kati (Central), kwa siku saba, huku jeshi hilo likidai kuwa linamshikilia kwa kuchapisha habari za uchochezi kwenye mitandao ya kijamii, kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.

Hata hivyo, hakuna kosa hata moja miongoni mwa makosa hayo yaliyotajwa awali na polisi, ambayo Kabendera ameshitakiwa mahakamani leo.

Kabendera amekuwa akiandika makala zake katika magazeti mbalimbali, ikiwamo gazeti la Uingereza la The Economist.

Miongoni mwa makala zinazodaiwa kuandikwa na Kabendera, ni pamoja na ile iliyopewa kichwa cha maneno kisemacho, “Another critic of President John Magufuli is silenced” – Mkosoaji mwingine wa Rais Magufuli anyamazishwa. Habari hii ilichapishwa kwenye gazeti hilo mashuhuri la nchini Uingereza na maeneo mengine ulimwenguni.

Mbali na kufanya kazi ya uandishi wa habari, Erick Matuga Kabendera, amekuwa akifanya kazi za ushauri wa masuala mbalimbali ya kiuchumi na kisiasa na Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na baadhi ya balozi zilizopo nchini.

Kabla ya kukamatwa na polisi, Kabendera alikuwa ameshikiliwa kwa madai ya uraia wake.

Hatua ya Polisi kudai kuwa limemkamata na kumshikilia mwandishi huyo mashuhiri wa magazeti yanayochapishwa kwa lugha ya Kiingereza,  kutokana na madai ya uraia wake, kuliibua mjadala mpana miongoni mwa makundi ya waandishi wa habari, ikiwamo sababu ya polisi kujiingiza kwenye kutaka kufahamu suala la uraia wa mwandishi huyo, wakati kazi hiyo hufanywa na Idara ya Uhamiaji.

Sakata la uraia wa Kabendera, liliibuka kwa mara ya kwanza mwaka 2013, lakini baadaye mamlaka nchini humo zilithibitisha kuwa Kabendera ni raia halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

Mataifa Afrika Mashariki yawasilisha bajeti 2024/2025 inayolenga kukuza uchumi

Spread the loveMataifa manne ya Afrika Mashariki jana Alhamisi yamewasilisha bungeni bajeti...

Habari za SiasaTangulizi

Gesi asilia, petroli kodi juu

Spread the loveWaziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amependekeza kufanya marekebisho kwenye...

Habari za SiasaTangulizi

Bilioni 155.4 kugharamia kicheko cha wastaafu 2022-2030

Spread the loveWaziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema jumla ya Sh...

error: Content is protected !!