Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mnyika awakabidhi Bawacha zigo la katiba mpya, tume huru
Habari za SiasaTangulizi

Mnyika awakabidhi Bawacha zigo la katiba mpya, tume huru

Spread the love

 

BARAZA la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), nchini Tanzania, limepewa jukumu la kupigania upatikanaji wa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Bawacha limekabidhiwa jukumu hilo, leo Jumanne tarehe 18 Mei 2021, na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, katika Mkutano wa Kamati Tendaji yake, uliofanyika jijini Mwanza kwa ajili ya kuchagua viongozi wa baraza hilo.

Viongozi wa Bawacha watakaochaguliwa na kamati hiyo, ni Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Zanzibar pamoja na Katibu Mwenezi.

Uchaguzi huo umeitishwa kufuatia waliokuwa viongozi wake, kufukuzwa uanachama wa Chadema, kwa makosa ya usaliti, tarehe 27 Novemba 2020.

Sharifa Suleiman, Makamu Mwenyekiti wa Bawacha-Zanzibar

Akizungumzia uchaguzi huo, Mnyika amewatahadharisha viongozi watakaochaguliwa, jukumu lao halitakuwa kusaka nafasi za uteuzi wa viti maalum vya ubunge na udiwani, bali ni kutafuta tume huru na katiba mpya.

“Viongozi mtakaowapata leo wana kazi kubwa, sio tu kufikiria kwamba Bawacha ni baraza la viti maalum vya ubunge na udiwani. Wajue ni baraza la kazi ya kutetea wanawake, kutafuta tume huru na katiba mpya ya nchi yetu,” amesema Mnyika.

Katibu Mkuu huyo amesema, viongozi hao watakaochaguliwa wana majukumu mazito mbele yao, kuhakikisha Tanzania inarudi katika misingi ya demokrasia, haki na utawala bora.

Wanawake walioteuliwa na Kamati Kuu ya Chadema kugombea Ukatibu Mkuu wa Bawacha, Asia Msangi, Catherine Ruge na Esther Daffi. Nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Grace Tendega.

Kwa upande wa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bawacha Bara iliyokuwa inashikiliwa na Jesca Kishoa, walioteuliwa kugombea ni Brenda Rupia Jonas, Emma Theobald Boki na Nuru Elias Ndosi.

Huku nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bawacha Zanzibar, akiteuliwa Bahati Chum Haji, kugombea peke yake.

Nafasi ya Katibu Mwenezi iliyokuwa inashikiliwa na Agnesta Lambart, walioteuliwa kugombea ni, Aisha Machano Ame, Husna Amri Said na Sigrada Wilhem Mligo.

Waliokuwa viongozi wa Bawacha wakiongozwa na Halima Mdee (aliyekuwa Mwenyekiti), Hawa Mwaifunga (Makamu Mwenyekiti) na wanachama wengine wa Chadema 17, walifukuzwa uanachama chama hicho tarehe 27 Novemba 2020, siku tatu baada ya kuapishwa kuwa wabunge viti maalum.

Mdee na wenzake waliapishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kushika nafasi hizo tarehe 24 Novemba 2020, kinyume na msimamo wa Chadema wa kutowasilisha wawakilishi wake bungeni, kikipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Kwa sasa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bawacha Zanzibar, Sharifa Suleiman, anakaimu nafasi ya Uenyekiti wa baraza hilo.

Kuhusu nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bawacha Bara, Mnyika amesema, nafasi hizo zitajazwa katika Mkutano Mkuu wa baraza hilo, utakaoitishwa hivi karibuni.

“Mamlaka ya kikatiba ya kuchagua na kuziba moja kwa moja yapo mbele ya mkutano mkuu wa Bawacha, kwa mujibu wa muongozo wa Bawacha,” amesema Mnyika.

Mbali na Mdee waliofukuzwa, wengine ni, waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko, pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.

Katika orodha hiyo, wamo pia Hawa Subira Mwaifunga, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara); Agnesta Lambat, aliyekuwa katibu mwenezi na Asia Mwadin Mohamed, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar na Katibu Mkuu, Bawacha-Bara, Jesca Kishoa

Pia, aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.

Wengine waliofukuzwa Chadema, Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

error: Content is protected !!