
David Silinde, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
SERIKALI iko katika hatua za mwisho kulifanya eneo la Mlima Nkongore mkoani Mara, kuwa hifadhi ya Taifa. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa tarehe 21 Mei 2021, bungeni jijini Dodoma, na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, David Silinde, akimjibu Mbunge wa Tarime Mjini (CCM), Mwita Michael, aliyehoji taratibu zilizotumika kuchukua ardhi hiyo kutoka kwa wananchi, na kulikabidhi kwa Jeshi la Magereza.
“Halmashauri ya Mji Tarime kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, inakamilisha taratibu za kulifanya eneo la Mlima Nkongore kuwa hifadhi,” amesema Silinde.
Silinde amesema wananchi walinyang’anywa eneo hilo, baada ya kubainika wanafanya shughuli za kiuchumi zinazohatarisha mazingira ya Mlima Nkongore.
“Wananchi wanaozunguka eneo hilo walikuwa wakiutumia mlima huo kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo ukataji kuni, uchomaji mkaa na kilimo, shughuli ambazo zilikuwa zinahatarisha mazingira yake,” amesema Silinde.
Pia, Silinde amesema eneo la mlima huo lilikuwa halijamilikishwa kwa wananchi kisheria na wala halikuwa na mipango miji.
“Mlima Nkongore una eneo lenye ukubwa wa ekari 266.65, eneo hilo halina mchoro wa mipango miji na halijamilikishwa,” amesema Silinde.
More Stories
Chongolo atoa siku 60 kwa MSD kupeleka vifaatiba hospitali Ushetu
NMB yafadhili wiki ya unywaji maziwa Katavi
#LIVE: Tuzo za EJAT2021, Majaliwa atoa ujumbe kwa MCT