May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Changamoto za afya: Mbunge CCM awapigania wahitimu vyuo vikuu

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Khamis

Spread the love

 

MBUNGE wa Viti Maalum (CCM), Latifa Juakali ameishauri Serikali ianzishe huduma ya bima ya afya, kwa wanafunzi wa elimu ya juu na wahitimu wanaosubiri kupata ajira, ili waondokane na changamoto za kumudu gharama za huduma ya afya. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).

Juakali ametoa ombi hilo leo Ijumaa tarehe 21 Mei 2021, bungeni jijini Dodoma, katika kipindi cha maswali na majibu.

“Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kuwapatia Bima ya Afya, wanafunzi wa
Elimu ya Juu na wanaosubiri kupata ajira?” amesema Juakali.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Khamis, amesema Serikali iko mbioni kuwasilisha bungeni muswada wa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, ili wanafunzi hao wanufaike na bima hizo.

“Kwa kutambua umuhimu wa kila mwananchi kuwa na Bima ya Afya, Serikali inakamilisha Rasimu ya Muswada wa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Ambao utawasilishwa Bungeni mwezi Juni 2021,” amesema Mwanaidi.

Aidha, Mwanaidi amesema Serikali inatekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu, ambao hujiunga kwa kuchangia na kunufaika na huduma za bima ya afya kwa mwaka mzima.

Chuo Kikuu cha Dodoma

“Serikali imeendelea kuboresha huduma za bima ya afya, kwa kuongeza kitita cha huduma na upatikanaji wa huduma kwa wanachama kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kwa kutekeleza mikakati mbalimbali yenye lengo la kuwawezesha wananchi wengi kujiunga na hivyo kuwa na uhakika wa kumudu gharama za matibabu,” amesema Mwanaidi.

Kuhusu wahitimu wanaosubiri kupata ajira, Mwanaidi amesema Serikali imeandaa utaratibu wa vifurushi vinavyowawezesha kupata bima hiyo.

“Kwa wale wanaosubiri kupata ajira, Mfuko umeandaa utaratibu wa Vifurushi ambavyo vimezingatia uhitaji wa aina ya huduma, umri na ukubwa wa familia. Kwa kumpatia mwananchi wigo wa kuchagua aina ya kifurushi kwa kulingana na mahitaji yake,” amesema Mwanaidi.

error: Content is protected !!