Saturday , 27 April 2024
Home Kitengo Maisha Elimu Mitihani kidato cha sita Juni 29, Prof. Ndalichako atoa maagizo
ElimuTangulizi

Mitihani kidato cha sita Juni 29, Prof. Ndalichako atoa maagizo

Wanafunzi wakifanya mtihani
Spread the love

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako amesema, mitihani ya kidato cha sita mwaka 2020 itaanza Juni 29 hadi Julai 16, 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Awali, mitihani hiyo ilikuwa ifanyike kuanzia tarehe 4 Mei 2020 lakini ikasitishwa baada ya Serikali ya Tanzania kutangaza kuzifunga shule zote za msingi na sekondari kuanzia tarehe 17 Machi, 2020 ili kuepusha kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19).

Hatua hiyo ya kuzifunga shule hizo, ilitokana na kuripotiwa kwa mgonjwa wa kwanza wa corona tarehe 16 Machi 2020 jijini Arusha.

Jana Alhamisi, Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli akizungumza baada ya kumaliza kuwapisha viongozi mbalimbali Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, alitanmgaza kufunguliwa kwa vyuo na wanafunzi wa kidato cha sita kuanzia tarehe 1 Juni 2020.

Baada ya maagizo hayo ya Rais Magufuli, leo Ijumaa tarehe 22 Mei, 2020 jijini Dodoma, Profesa Ndalichako amezungumza na waandishi wa habari ambapo ametoa maelekezo kwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Profesa Ndalichako amesema, shule zinapaswa kuanza maandalizi mapema ili kuanzia tarehe 30 Mei, 2020 wanafunzi wanaosoma shule za bweni waanze kuripoti ili ikifika tarehe 1 Juni, 2020 masomo yaanze rasmi.

Amesema, shule za kutwa nazo zianze maandalizi mapema kama ambavyo Rais Magufuli ameelekeza, “na nisisitize kwamba, shule ambazo zinafunguliwa ni za kidato cha sita tu.”

Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu

Kuhusu mitihani ya kidato cha sita amesema, Profesa Ndalichako amesema, “baada ya kufunguliwa, wanafunzi watajisomea hadi tarehe 28 Juni, 2020 na mitihani itaanza rasmi tarehe 29 Juni hadi 16 Julai, 2020 na mitihani hii itakwenda sambamba na mitihani ya walimu.”

“Natoa wito kwa baraza la mitihani kusabambaza ratiba ya mitihani hii na ihakikishe mitihani hii matokeo yake yatoke kabla ya tarehe 31 Agosti 2020 ili kutokuathiri mihula ya vyuo vikuu,” amesema Profesa Ndalichako.

Amesema, baada ya kutoka kwa matokeo, wanafunzi watapata fursa ya kufanya maombi katika vyuo mbalimbali wanavyovipenda.

Kuhusu vyuo vikuu na vya kati, Profesa Ndalichako ameviagiza vyuo kufanya maandalizi na mamlaka za vyuo vikuu kwa maana ya mabaraza na seneti kuhakikisha masoma yanaendeshwa kwa kufidia muda ambao vyuo vilikuwa vimefungwa.

“Ni lazima, ratiba zibadilike ili kuwe na muda zaidi wa kusoma ili kufidia,” amesema.

Waziri huyo amesema, mabaraza pamoja na seneti za vyuo zinapaswa kuweka utaratibu huo na zinawasilishe mabadiliko hayo kwa tume ya vyuo vikuu na Nacte ifikapo tarehe 27 Juni 2020 ili kufahamu wamepanga nini ili bodi ya mikopo ifahamu ratiba ya kila chuo.

“Tunasisitiza kwamba, hakutakuwa na muda wa ziada, ratiba zao ziweze kufidia ili kutokuathiri mzunguko wa masomo mwaka ujao,” amesema waziri huyo.

Kuhusu mikopo, Profesa Ndalichako amesema, kama alivyosema Rais Magufuli wajiandae, “ningependa kuwahakikishia Watanzania kwamba, fedha kwa ajili ya kulipa tunazo Sh.122.8 bilioni.”

Profesa Ndalichako ameviagiza vyuo ifikapo tarehe 28 Mei, 2020 vyuo vyote viwe vimewasilisha nyaraka muhimu bodi ya mikopo ili kufikia tarehe 30 Mei, 2020 fedha ziwe zimetolewa kwani fedha zipo.

“Mara nyingi ucheleweshaji umekuwa ukitokea vyuo, wanafunzi wamekaa nyumbani muda mrefu na sitarajii kuona usumbufu ukitokea na vyuo vijipange ikiwemo kuweka maofisa wa kutosha vyuoni,” amesema Profesa Ndalichako.

Pia, ameagiza viongozi wa vyuo na shule kuhakikisha wanaweza mazingira salama ya kujikinga na corona ikiwamo maeneo ya kunawa mikono kwa maji tiririka.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

error: Content is protected !!