Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mbunge Nditiye azikwa, ujumbe watolewa
Habari za Siasa

Mbunge Nditiye azikwa, ujumbe watolewa

Spread the love

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema, sifa na maneno mazuri ambayo yamesemwa kuhusu aliyekuwa Mbunge wa Muhambwe (CCM), Mhandisi Atashasta Nditiye yatakuwa na maana tu endapo matendo mema aliyoyatenda wakati wa uhai wake yataenziwa na kuendelezwa. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Majaliwa amesema hayo jana Jumatatu tarehe 15 Februari 2021, katika Ibada ya kumwombea marehemu Nditiye, iliyofanyika Kanisa la Anglikana la Kibondo, mkoani Kigoma.

Waziri mkuu alisema, Serikali inathamini mchango alioutoa wakati wa uhai wake na ndiyo maana Rais John Magufuli amemtuma amwakilishe katika maziko hayo.

Aliwataka wana-Muhambwe, wabunge na Watanzania kwa ujumla, wamwombee marehemu Nditiye ili Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi.

“Nawasihi tuwe karibu na familia ya marehemu kama tulivyokuwa wakati wa uhai wake, hatua ambayo naamini itawapa faraja wanafamilia,” amesema.

Naye, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson alisema, Spika Job Ndugai amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Nditiye kwani alikuwa na mchango mkubwa katika Bunge kutokana na michango yake mizuri ya uzalendo, mapenzi makubwa kwa wapiga kura wake na Taifa pia.

“Kwa mara ya mwisho, Mhandisi Nditiye alichangia katika Bunge lililopita tarehe 9 Februari, 2021 wakati nikiwa kwenye kiti na hakuna aliyedhani kuwa leo tusingekuwa naye. Niwasihi ndugu zangu tuwe tayari wakati wote kwani hakuna ajuaye siku yake ya mwisho,” alisema.

Mwakilishi wa Wabunge wa Mkoa wa Kigoma ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alisema anaishukuru Serikali hasa Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
kwa misaada waliyoitoa wakati wa kumuuguza, wakati wa msiba na katika mazishi.

Aliishukuru pia Ofisi ya Bunge ikiongozwa na Spika Ndugai, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai na wabunge wote kwa ushiriki wao wa hali na mali katika ugonjwa, msiba na mazishi ya Mhandisi Nditiye.

Akitoa salamu zake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye alisema Mhandisi Nditiye alitumia muda wake mwingi kukutana na viongozi wa mkoa huo ili kujadili na kushauriana masuala mbalimbali yaliyohusu maendeleo ya mkoa huo.

Mhandisi Nditiye alizaliwa 17, Oktoba 1969 wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.

Alisoma shule ya msingi Kabwigwa kuanzia mwaka 1975 hadi 1981 na baadaye alijiunga na Chuo cha Ufundi Dar es Salaam ambako alisoma kuanzia mwaka 1984 hadi 1986 na kutunukiwa cheti cha uhandisi.

Katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli, Mhandisi Nditiye alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano.

Taarifa ya kifo chake ilitolewa Bungeni tarehe 12 Februari 2021 na Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye alisema kuwa kifo hicho kimetokana na ajali aliyoipata Jumatano, 10 Februari 10, 2021 katika eneo la Nanenane, jijini Dodoma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!