May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi Tanzania wamkamata Askofu Mwamakula

Spread the love

 

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam nchini Tanzania, linamshikilia, Emmaus Mwamakula, Askofu wa kanisa la Uamsho la Moravian kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano nchi nzima yenye lengo la kudai katiba mpya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa ya Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, aliyoitoa usiku wa tarehe 15 Februari 2021, imesema Askofu Mwamakula ametumia mitandao ya kijamii, kuhamasisha maandamano.

“Taarifa ilikuwa ikihamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi ili kuandamana wakishinikiza na kudai katiba mpya jambo ambalo ni kinyume na taratibu na sheria za nchi,” amesema Mambosasa

“Aidha awali, Jeshi la Polisi kupitia idara ya upelelezi kanda Maalum Dar es Salaam, walifanikiwa kupata taarifa hiyo na kumkamata Askofu huyo kwa ajili mahojiano kwa jambo hilo ambalo lilileta taharuki kwa umma katika mitandao ya kijamii.”

Mambosasa amesema “Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa yeyote ambaye ameshawishika na kupanga kuandamana kuahirisha mara moja nia hiyo ovu ambayo iko kinyume na sheria.”

“Pia ifahamike ni kosa kufanya maandamano bila kuwa na kibali cha Polisi ili kupewa ulinzi, na atakayejaribu kuandamana atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Hivyo wananchi wote wa jiji la Dar es Salaam, waendelee na shughuli zao za kukuza uchumi na kujipatia vipato vyao vya kila siku,” amesema.

error: Content is protected !!