Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kikwete: Nimempoteza mtu wa karibu katika maisha yangu
Habari za SiasaTangulizi

Kikwete: Nimempoteza mtu wa karibu katika maisha yangu

Spread the love

 

RAIS mstaafu wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amesema, taifa limempoteza mzalendo wa dhati na mtetezi shupavu wa Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Mohammed Seif Khatibu. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Dk. Mohammed Seif Khatibu (70), aliyehudumu katika nafasi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), tangu mwaka 1978, alifikwa na mauti jana Jumatatu, tarehe 15 Februari 2021, katika Hospitali ya Al Rahma, Kilimani, Unguja, alikokuwa akipatiwa matibabu.

“Taifa limepoteza mzalendo wa dhati na mtetezi shupavu wa Mapinduzi ya 1964.”

Mwili wake, umezikwa leo Jumanne, kijijini kwake, Uzini, Unguja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mmoja wa wanafamilia wake, swala ya maiti ilifanyika katika msikiti wa Mchina, Mpandae.

Akiwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Kikwete, amezungumzia safari ya maisha ya Dk. Khatibu ambaye ni miongoni mwa wanasiasa aliofanya nao kazi kwa karibu.

Akiandika katika ukurasa wake wa Twitter, Kikwete ameeleza na kuonesha picha zilizoashiria namna ‘alivyoshibana’ na Dk. Khatibu.

Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi akiongoza mazishi yaDk. Mohamed Seif

“Nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Comrade Mohamed Seif Khatibu. Nimepoteza rafiki wa karibu wa tangu ujana hadi uzee wetu. Tumefahamiana naye tangu mwaka 1982 tulipochaguliwa kwenye uongozi wa taifa wa UV-CCM” (Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi).

Amesema, baada ya vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shiraz Party (ASP), kuungana mwaka 1977, ambako Dk. Khatibu alifanywa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UV-CCM), wamekuwa wote kwa shida na raha.

“Baada ya kuunganishwa TANU Youth League na ASP Youth yeye akawa mwenyekiti wa kwanza wa taifa na mimi nikiwa miongoni wa wajumbe wa kwanza wa kamati ya utekelezaji ya taifa. Tangu wakati huo, mpaka sasa, amekuwa mtu wangu karibu katika maisha yangu ya kisiasa na hata kijamii,” ameeleza Kikwete.

Amesema, “tarehe 8 Novemba 1988, tuliteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuingia kwenye baraza la mawaziri. Yeye alikuwa waziri wa Nchi Ofsi ya Makamu wa Pili wa Rais na mimi nikawa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.”

Viongozi wa Serikali ya Zanzibar wakiwa kwenye ibada ya kumswalia Dr Mohammed Seif

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, kutokana na msiba huo mkubwa na wa kushutikiza, “CCM kimepoteza moja wa makada wake mahiri na jasiri.”

Akihitimisha maelezo yake, Rais Kikwete amewatakia wana familia wa mwanasiasa huyo, moyo wa subira na ustahamilivu. Amemtakia na kumuombea marehemu mapumziko mema peponi.”

Mpaka anakutwa na mauti, Dk. Khatibu alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) na mmiliki na mkurugenzi wa kampuni ya Zanzibar Media Group inayomiliki kituo cha Redio cha Zenj FM, televisheni ya Zenji TV na gazeti la Nipe Habari.

Katika maisha yake ya siasa, Dk. Khatibu alikuwa mtu wa karibu na mtiifu kwa Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania. Alikuwa mjumbe katika Umoja wa Vijana Tanzania (UVT) kabla ya kubadilisha na kuwa UV-CCM.

Alikuwa waziri katika wizara mbalimbali katika serikali ya Muungano na mbunge wa Uzini, Unguja.

Aidha, Dk. Khatibu alikuwa mshairi na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Aliwahi kuwa mwanasoka aliyechezea klabu ya mpira wa miguu ya Kikwajuni, Zanzibar na timu ya Taifa ya Zanzibar. Dk. Khatibu aliwahi pia kuimba taarabu.

Wakati wa mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za wagombea urais ndani ya CCM, mwaka 2015, Dk. Khatibu akiwa mkuu wa Oganizesheni wa chama hicho, alikuwa na jukumu la kuwapatia fomu wagombea wote waliojitokeza kuwania urais, akiwemo Dk. John Magufuli.

Dk. Khatibu amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashuari Kuu (NEC) ya CCM, kati ya mwaka 1978 hadi 2017. Amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kati ya mwaka 1995 hadi 2017. Amekuwa katibu wa  Oganaizesheni kati ya mwaka 2012 na 2017.

Atunukiwa shahada ya uvamivu (PhD), katika chuo kikuu cha UDOM, tarehe 25 Novemba 2011, akiwa mwanafunzi wa kwanza kutunukiwa shahada hiyo katika chuo hicho.

Alitunukiwa shahada yake na aliyekuwa mkuu wa chuo hicho, rais mstaafu, Benjamin Willim Mkapa. Kwa sasa, Mkapa naye ni marehemu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!