December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge ahoji vitisho vya polisi

Devotha Minja, Mbunge wa Viti Maalum Chadema

Spread the love

DEVOTHA Minja, Mbunge wa Viti Maalum mkoani Morogoro (Chadema), ameeleza kukerwa na kauli za vitisho zinazotolewa na Jeshi la Polisi nchini. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Amehoji sababu za polisi kujenga utamaduni wa kutoa vitisho kwa wananchi ambapo ndio wanaolipa kodi inayotumika kuwapa mishahara.

Mbunge huyo ameuliza swali leo tarehe 9 Aprili 2019 bungeni jijini Dodoma, akiitaka Wizara ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI kutoa tamko kuhusu kauli iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa iliyolenga kuonya watu waliotangaza nia ya kuandamana.

“Si wakuu wa mikoa na wilaya ambao hawafanyi vizuri, wapo pia MaRPC hawafanyi vizuri, RPC anaposema wananchi wakiandamana wanapigwa hadi wachakazwe, hivi anavyolipwa mshahara kazi ni kuchakaza wananchi?” amehoji Minja.

Akijibu swali la Minja, Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Suleiman Jaffo amesema vyombo vya dola vinaendeshwa kwa kanuni na sheria zake, hivyo serikali haiwezi kuviingilia na kuwataka wananchi kufuata sheria ili kuepuka migogoro.

“Jambo la kwanza, tuweke ushirikiano kila eneo, vyombo vingine vinaendeshwa kwa kanuni, hatuwezi kuingilia mambo yao ya ndani. Ni vyema wananchi wakafuata sheria ili kuondoa migongano,” amesema Jaffo.

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alihoji ukimya wa serikali kuhusu vitendo vya baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa wanaodaiwa kuwanyanyasa wananchi .

“Wilaya ya Hai mkuu wa wilaya bado anaendelea na vitendo vya kukamata wananchi na wawekezaji na kuwatumia maskari kushawishi wanasiasa wahame vyama vyao, sasa ningependa kujua baada ya kauli za waziri ni hatua zipi serikali imepanga kuchukua,” amehoji Selasini.

Akijibu swali la Selasini, Jaffo amesema “Ttumetoa maelekezo kwa watu wetu kwa kuwa wamepewa dhamana, kitendo hicho si sawa sawa jukumu letu sasa kuwachukulia hatua na rais ametoa maagizo.”

error: Content is protected !!