LIVINGSTON Lusinde, Mbunge wa Jimbo la Mtera (CCM), ameshauri bunge na wananchi kwa ujumla kwamba, kusiwepo na uchaguzi wa rais mwaka 2020. Anaripoti Danson Tibason, Dodoma…(endelea).
Ameshauri, kuwepo na uchaguzi wa wabunge na madiwani pekee kwa kuwa, hakuna mtu anayeweza kupambana na Rais John Magufuli ngazi ya urais kwenye uchaguzi huo.
Lusinde ametoa kauli hiyo bungeni tarehe 9 Aprili 2019 wakati akichangia hoja ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuhusu mwelekeo wa kazi za serikali na mapato na matumizi ya ofisi yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2019/20.
“Mimi nawaomba wabunge na Watanzania wote, hivi kwanini mwakani tusifanye uchaguzi wa madiwani wabunge tu na Rais akapita bila kupingwa? Kwanini tusifanye hivyo?” amesema Lusinde na kuongeza;
“Kwanza, tutakuwa tumeokoa fedha nyingi sana, wakati rais anaapishwa tumkabidhi cheki ya fedha ambazo taifa limeokoa, ili aende kuzitumia kuondoa matatizo ya maji na barabara vijijini.”
Mbunge huyo wa Mtera amesema, hakuna sababu ya kutumia fedha nyingi kumchagua rais kwa kuwa, aliyepo hana mpinzani.
“Kuna faida gani kwenda kupoteza fedha kwa uchaguzi wa rais ambaye hana mpinzani? Kwa faida gani? Naomba mitandao yote, wanazuoni wote hoja hii naiweka mezani, tuangalie faida ambayo nchi itapata kwa kufanya uchaguzi na hasara zake ili tupime. Sisi ni wabunge, tunaotokana na familia masikini tusijisahau.
“Watu maskini wanajinyima, badala ya kula milo mitatu wanakula mlo mmoja, kwanini na sisi tusijinyime kwa kula mlo wa madiwani, mlo wa wabunge na rais apite bila kupingwa?” amehoji.
Akifafanua zaidi amesema, aliyekuwa mshindani mkubwa wa Rais Magufuli kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, tayari amerejea CCM hivyo, hakuna mshindani mwingine mwenye nguvu.
“Mshindi namba mbili ‘ulipo tupo’ (Edward Lowassa) tayari yuko kulekule na wengine wamemfuata hukohuko.
“Hivi kuna chama katika nchi hii kinaweza kumtengeneza mgombea urais ndani ya miezi tisa na akamshinda Rais Magufuli?” ameshoji na kujibu “Haiwezekani.”
Leave a comment