RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Dk. Oscar Mbyuzi. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).
Taarifa ya utenguzi huo imetolewa leo tarehe 9 Aprili 2019 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa.
Taarifa ya Msigwa inaeleza kuwa, Rais Magufuli amemteua Jimson Mhagama kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa.
“Uteuzi wa Bw. Mhagama unaanza mara moja leo tarehe 9 Aprili 2019,” inaeleza sehemu ya taarifa ya Msigwa.
Hata hivyo, taarifa ya Msigwa haikueleza sababu za utenguzi wa Mbyuzi.
Hatua hiyo ya Rais Magufuli imekuja siku moja baada ya kiongozi huyo mkuu wa nchi kumaliza ziara yake ya kikazi ya siku sita mkoani Ruvuma.
Katika ziara yake hiyo mkoani Ruvuma iliyoanza tarehe 4 hadi 9 Aprili mwaka huu, Rais Magufuli alizindua miradi mbalimbali ikiwemo barabara ya Tunduru-Matemanga-Namtumbo, pamoja na ujenzi wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wilayani Namtumbo.
Leave a comment