September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbivu, mbichi za Membe, Kinana, Makamba 

Spread the love

TAARIFA ya matokeo ya mahojiano yaliyowahusu Bernard Membe, Abdulrahman Kinana na Mzee Yusuph Makamba, inayosubiriwa kwa hamu kubwa nadani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inakaribia kutoka. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inatarajia kuwasilisha taarifa yake ya mahojiano kuhusu tuhuma za wanasiasa hao kuhusu utovu wa nidhamu katika Kamati Kuu, mwishoni mwa wiki hii.

Taarifa hiyo imetolewa na Dk. Bashiru Ally wakati akizungumza na wanahabari leo tarehe 24 Februari 2020 jijini Dodoma, imeeleza jambo hilo linakaribia tamati.

Dk. Bashiru amesema, kwa sasa maandalizi ya taarifa za mahojiano ya makada hao ambao ni Bernard (Waziri wa Mambo ya Nje Mstaafu), Abdulrahman Kinana na Mzee Yusuph Makamba (makatibu wakuu wastaafu), yako katika hatua za mwisho.

“Napenda kuwataarifu kwamba, ndani ya siku saba zilizotolewa na Kamati Kuu, ilikuwa imeshakamilisha taarifa yake, siku ya Jumatano wiki hii Kamati Ndogo ya Nidhamu na Maadili chini ya Mzee Mangula, itakua inapitia taarifa yake kwa ajili ya kuwasiliha kwenye vikao vya Kamati ya Usalama na Maadili na Kamati Kuu,” amesema Dk. Bashiru na kuongeza:

“Bado tunapanga vizuri baada ya Jumatano ili kabla ya mwisho wa wiki hii kwa ajili ya kupokea ripoti ya Mangula.”

Dk. Bashiru amesema, taarifa hiyo iliyotarajiwa kuwasilishwa kwenye kikao cha Kamati Kuu tarehe 19 Februari 2020, ilichelewa kwa sababu ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo kubanwa na majukumu ya kazi za chama.

“Imechukua muda tangu siku saba kukamilika tarehe 19, lakini maelekezo ya viongozi wakuu hasa mwenyekiti wa chama, Mangula alikuwa na kazi aliyopewa na kamati kuu ya kwenda kuzindua jengo la Makao Makuu ya chama mkoani Geita, na kufanya ziara Tabora, Shinyanga na Singida,” amesema Dk. Bashiru.

Sakata la makada hao watatu wa CCM kuhojiwa kwa utovu wa nidhamu, lilianza kuibuka baada ya kuvuja kwa sauti za mazungumzo yanayodaiwa kuwa ni yao, ambapo maudhui yake yalikuwa kukosoa baadhi ya viongozi wa chama hicho na wa serikali.

Sauti hizo zilivuja katika nyakati tofauti mwaka jana, baada ya Mzee Makamba na Kinana kuandika waraka uliopinga wastaafu kudhalilishwa pasina mamlaka husika kuwachukulia hatua wanaodhalilisha wastaafu hao.

error: Content is protected !!