April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

A-Z kilichotokea kesi ya kabendera

Spread the love

SAFARI chungu ya Erick Kabendera, mwandishi wa habari za uchunguzi kitaifa na kimataifa, katika kesi ya uhujumu uchumi imetamatika leo tarehe 24 Februari 2020. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam…(endelea).

Tamati ya safari yake imifika leo kutokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imemwacha huru Kabendera baada ya kutekeleza masharti ya kulipa fidia ya Sh. 250,000 kwa kosa la kukwepa kodi na Sh. 100 milioni kwa kosa la kutakatisha fedha.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kabendera kukiri mahakamani hapo kosa la kukwepa kodi na utakatishaji fedha. Hata hivyo, mahakama hiyo imemtaka kulipa fidia ya Sh. 172 milioni katika kipindi cha miezi sita tangu siku aliyoachwa huru.

Kabendera alikamatwa tarehe 29 Julai  2019 na kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza tarehe 5 Agosti 2019, ambapo amepandishwa kizimbani mara 19 bila upelelezi kukamilika. 

Jinsi ilivyokuwa

Upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Reginald Martin na Wakili Jebra Kambole ambapo Mwanasheria Paul Kisabo alikuwepo mahakama kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa kesi hiyo. 

Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili wawili, Faraja Nchimbi na Wakili Wankyo Simon. 

Wakili Faraja Nchimbi alianza kwa kuiambia mahakama kwamba, mshitakiwa Erick Kabendera yupo mahakamani na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), ameridhia maombi ya kukiri kosa yaliyowasilishwa na mshitakiwa kwa mujibu wa kifungu Na. 26(1) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200.

Wakili Nchimbi amesema, kwamba DPP ameipa hati mahakama kusikiliza shauri hili la uhujumu uchumi kwa mujibu wa kifungu namba 12(3)& (4) cha sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200. 

Wakili Nchimbi amesema kwamba DPP amethibitisha kuridhia kuingia katika makubaliano ya kukiri kosa (Plea Agreement) na Mshitakiwa Erick Kabendera kwa mujibu wa kifungu namba 194 C (3).

Pia wakili Nchimbi amewasilisha nakala ya makubaliano (Plea Agreement), mbele ya mahakama ambayo imesainiwa na Wakili Nchimbi kwa niaba ya DPP, mshtakiwa Kabendera, dada yake Prisca Kabendera pamoja na wakili wake Jebra Kambole.

Hakimu Janet Mtega amesema, kwamba kwa mujibu wa kifungu namba 198(A) (1)&(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20, “nimepokea nakala hizo.”

Wakili Nchimbi amesema kwamba, kwa mujibu sehemu B aya ya 6 ya Mkataba wa Makubaliano (Plea Agreement), DPP ameridhia kuondoa kosa la kwanza la kuongoza genge la uhalifu. 

Wakili Nchimbi amesema, kwa mujibu wa kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 “naiomba kuifahamisha mahakama, kwamba tumeondoa shitaka la kwanza na hivyo kubakiwa na shitaka la pili na la tatu.”

Baada ya hapo Kabendera aliapishwa kwa mujibu wa kifungu namba 194 E (i) cha Sheria ya Mwenedo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 na kuelezwa matokeo ya kiapo chake juu ya kukiri kosa kuwa hawezi kukata rufaa juu ya kile ulichokiri isipokuwa anaweza kukata rufaa kuhusu hukumu yake.

Wakili Nchimbi pia amesema, kwa mujibu wa kifungu namba 194 D (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20, kinahitaji mtuhumiwa kuonesha wazi utayari wake wa kukiri kosa ili mahakama iweze kutunza kumbukumbu.

Hakim Mtega alimuuliza Kabendera kama alitoa makubaliano hayo bila kulazimishwa, Kabendera amekiri mbele ya mahakama kuwa hakulazimishwa na mtu yeyote.

Baada ya hapo, Wakili Wankyo alimsomea Kabendera mashitaka mapya mawili ambayo ni: kushindwa kulipa kodi kiasi cha fedha taslimu za kitanzania Sh. 173 milioni kinyume na kifungu namba 105 (a) cha Sheria ya Kodi, kosa la pili ni kutakatisha fedha taslim za kitanzania millioni 173 kinyume na Sheria ya Uhujumu Uchumi. Kabendera akakiri makosa yake yote mawili. 

Wakili Nchimbi amesema, kwamba kwa mujibu wa kifungu namba 194 (1)(a)&(b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, mtuhumiwa anapaswa kusomewa masharti ya makubaliano yake na DPP.

Wakili Wankyo amesoma masharti hayo ambayo yanajumuisha makosa yake mawili aliyokiri, pamoja na ridhaa ya DPP juu ya maombi ya kukiri kosa. 

Masharti ya mkataba wa makubaliano na DPP ni kwamba, endapo Kabendera atakiuka masharti ya makubaliano hayo, DPP atakuwa na mamlaka ya kumfungulia mshitaka upya, yale ambayo yameondolewa wakati wa makubaliano ya kukiri kosa. 

Masharti mengine ni Kabendera anapaswa kulipa ndani ya miezi sita kwa awamu sita, na anapaswa kulipa kila tarehe 30 ya mwisho wa mwezi. Pia, atashirikiana na DPP kutoa taarifa zote za makosa yake.

Wakili wa Kabendera hakuwa na pingamizi lolote juu ya kilichowasilishwa mahakamani. 

Hakimu Mtega kabla ya kutoa hukumu, alimuuliza wakili wa serikali historia ya mshitakiwa. Wakili Nchimbi amesema, mashtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, “tunaiomba mahakama katika kutoa hukumu, ijielekeze Sehemu B aya 7 na 8 ya mkataba wa makubaliano wa kukiri kosa.” 

Wakili wa utetezi Jebra Kambole amesema, mahakama kabla ya kutoa hukumu izingatie kwamba, hii ni mara ya kwanza Kabendera kushitakiwa, tangu tarehe 5 Agosti 2019 mshitakiwa alikuwa magereza na amekuwa akifika mahakamani.

Pia ana familia inayomtegemea na afya yake sio njema, “tunaomba mahakama impatie adhabu ndogo na naiomba mahakama ijikite sehemu B aya ya 8 ya makataba wa makubaliano ya kukiri kosa.” 

Baada ya mawasilisho yote, Hakimu Mtega kwa mamlaka aliyopewa, amemtia hatiani Kabendera kwa makosa yote mawili aliyokiri. 

Kwa kosa la kwanza Hakim Mtega amemuhukumu Kabendera kulipa Sh. 250,000 na fidia ya Sh. 172 milioni. 

Kwa kosa la pili; Hakim Mtega amemuhukumu Kabendera kulipa Sh. 100 milioni.

error: Content is protected !!