FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, ‘wamealikwa’ kwenye meza ya mazungumzo na James Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Bila kuwataja majina, Mbatia amesema, anawaalika vyama vya siasa vya upinzani kuzungumzia ushirikiano kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktba 2020.
“Sina tatizo la kuwa na maridhiano na vyama vingine,” amesema Mbatia leo Alhamisi tarehe 4 Juni 2020, jijini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari.
“Kinachonipa shida na taabu, ni kuona baadhi ya wanasiasa wakitukana kwenye mitandao juu ya watu wanaohama chama kimoja kuingia chama kingine.”
Mbatia ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema kufungua milango ya ushirikiano na vyama vingine vya siasa nchini.
“Tunafungua mlango wa majadiliano na vyama ambavyo vinadhamira ya kweli ya kushirikiana kuiondoa CCM madarakani,” alisema Mnyika.
Chadema ndio chama kikuu cha upinzani nchini. Kwenye uchaguzi huo, zaidi ya vyama 15 vya upinzani vikiwemo CUF, ADC, UDP, UPDP, TADEA, TLP, UDP, CHAUSTA, PPT-MAENDELEO, SAU, ADC, CHAUMMA, AFP, CCK, NCCR-MAGEUZI, CHADEMA na ACT-WAZALENDO vinatarajiwa kushiriki.
Akizungumzi msimamo wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu, mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi na Mbunge wa Vunjo, Kilimanjaro amesema, kwenye siasa kinachosimama ni kushindana kwa hoja na si vinginevyo.
Mbatia amekumbusha kwamba, kupitia chama hicho Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliundwa na kwamba, chama hicho kinaamini kwenye ushirikiano na umoja.
“NCCR-Mageuzi ni kati ya vyama vya siasa ambavyo vinaamini kwenye ushirikiano. Hata Ukawa ni zao la NCCR. Naisitiza chama chetu kinaamini ushirikiano naumoja,” amesema.
Mwenyekiti huyo amesema, chama chake kinahamasisha vijana na akina mama kugombea nafasi mbalimbali za uchaguzi ndani ya chama hicho.
Ukawa ulianzishwa mwaka 2014 wakati wa Bunge Maalum la Katiba na ukaendelea katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2020.
Katika uchaguzi huo, Ukawa uliokuwa ukujumuisha vyama vya CUF, NLD, CHADEMA na NCCR-MAGEUZI vilishirikiana kwa kusimamisha wagombea mmoja katika kata, jimbo na urais.
Hata hivyo, baadhi ya kata na majimbo, haukufanikiwa kwani walisimama wagombea zaidi ya mmoja kutoka Ukawa
Leave a comment