December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanawake wanapenyaje uchaguzi mkuu 2020?

Spread the love

JOTO la uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 limeanza kufukuta, vyama mbalimbali vya siasa vimeanza kuweka mikakati yake ya kupata wagombea. Anaandika Mwandishi Wetu…(endelea).

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli hivi karibuni, amewataka wanachama wa chama hicho wanaotaka kugombea, kujitathmini na kujiridhisha kama wanatosha.

“Chama chetu kinayo demokrasia ya kutosha, lakini demokrasia hii ndani ya chama isije ikatumika kuleta fujo, kutugombanisha na kukiumiza chama, tuweke maslahi ya chama mbele na tutumie nafasi hii kukiimarisha chama chetu” alisema Rais Magufuli.

Chama kikuu cha upinzani nchini – Chadema – kupitia John Mnyika, Katibu Mkuu wake, kimetangaza kuanza mchakato kuelekea uchaguzi huo huku akiweka msimamo kwamba utovu wa nidhamu hatuavumiliwa. Vyama zaidi ya 16, vinatarajiwa kushiriki uchaguzi huo.

Wakati hayo yakiendelea, Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi chini ya uratibu wa Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania (WFT), umefanya uchambuzi wa sheria za uchaguzi Tanzania.

Kimantiki, sheria zenye kulinda haki na usawa wa binadamu huweka msingi imara wa utetezi wa haki hizo hususani haki za wanawake na makundi yaliyoko pembezoni.

Mwenyekiti wa WFT, Profesa Ruth Meena anasema, pamoja na kuwepo kwa sheria husika, chaguzi zote huendeshwa pia kwa kuzingatia  kanuni zinazotoa taratibu na masharti yanayotakiwa kuzingatiwa wakati wa uchaguzi.

Anasema, sheria zinazoongoza chaguzi ziko kwenye ngazi tatu, kimataifa, kikanda na kitaifa.

“Kwenye ngazi zote hizi, misingi ya usawa wa jinsia hubainishwa na hatima ya kuwataka wadau mbalimbali kuchukua hatua stahiki, ili kuwahakikishia wanawake na makundi yaliowekwa pembezoni ulinzi wa haki zao za kushiriki kwenye mchakato wa uchaguzi bila kubaguliwa kwa njia yoyote,” anasema.

Prof. Ruth Meena, Mwenyekiti wa WFT

Profesa Meena anasema, Serikali ya Tanzania imeridhia mikataba na kukubaliana na matamko mbalimbali yanayowajibisha washirika wazingatie katika kulinda haki za wanawake katika uchaguzi.

Amesema, nkutano wa Beijing ulibainisha maeneo 12 mahususi ya kufanyia kazi kwenye kupambana na ubaguzi wa jinsia.

Katika maeneo hayo 12, Tanzania ilibainisha maeneo ya awali manne ya kipaumbele ambayo ni wanawake na umaskini, uwezeshwaji kisheria, suala la uwezeshwaji kiuchumi na mtoto wa kike.

Anasema, kimantiki eneo la kurekebisha sheria zenye viashiria vya ubaguzi lilipewa kipaumbele tangu mwaka wa 1995, baada ya Mkutano wa Beijing.

Tamko la SADC

Profesa Ruth anasema, tamko la  Shirika la Maendeleo la Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) 2005, liliweka kiwango cha jinsia chini cha uwakilishi wa wanawake kuwa asili 30.

Baadaye kukipandisha kuwa asilimia 50 katika ngazi zote za uwakilishi na za maamuzi katika vyombo vya umma.

Anasema, wanachama washirika walihitajika kuchukua hatua, kuhakikisha usawa wa jinsia katika ngazi zote za maamuzi, kuwezesha wanawake kufikia na kumiliki rasilimali za nchi sawa na wanaume.

Pia, kubatilisha sheria zote kandamizi na zenye ubaguzi, kuhakikisha wanawake haki ya kupaa elimu sawa na wanaume na kuwahakikisha wanawake haki ya kuhabarishwa.

“Kimantiki, misingi ya usawa inayoongozwa na mikataba, matamko na miongozo ya kimataifa, na kikanda katika masuala ya uchaguzi ni pamoja na haki ya kutobaguliwa, haki ya kuchagua na kuchaguliwa, uhuru wa maoni na haki ya kuhabarishwa,” anasema Profesa Ruth.

Profesa Ruth anasema, katika ngazi ya taifa, misingi ya haki za wanawake katika uchaguzi, zinabainishwa kwenye Katiba ya nchi, sheria mbalimbali zinazohusu uchaguzi, kanuni na miongozo inayoelekeza utekelezwaji wa misingi husika.

Misingi hiyo ni pamoja na kutokubaguliwa kwa njia yoyote kwenye mchakato wa uchaguzi, haki ya kupiga kura, haki ya kuteuliwa, haki ya kufikia na kutumia rasilimali za uchaguzi, haki ya kuchaguliwa na uhuru wa kutoa maoni na haki ya kupata taarifa.

Waandishi wa habari

Profesa Ruth anasema, mfumo wa uchaguzi unaoongozwa na dhana ya “mshindi anapata yote” hauko rafiki kwenye kutekeleza azma ya msingi wa usawa na demokrasia shirikishi.

Anasema, wagombea wote kwenye mchakato wa uchaguzi lazima wawe wanachama wa vyama vya siasa na wawe wamependekezwa na vyama husika.

Kifungu cha 26 (2)(d) cha Katiba ya Zanzibar 2018) na Kifungu cha 36 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977).

“Kwenye muktadha unaoongozwa na mfumo dume ndani ya vyama na ambao uongozi hauna utashi wa kuzingatia azma ya usawa wa jinsia, sharti hili una athari mbaya zaidi kwa wanawake kuliko wanaume kutokana na ukweli, vyama vingi vinaongozwa na wanaume wasioonesha utashi wa kuleta mabadiliko ya kifikra yanayoongozwa na mfumo dume,” anasema.

Profesa huyo anasema, sheria haziko wazi kwenye mfumo wa uteuzi ndani ya vyama hususani kwenye kuzingatia msingi wa usawa uliobanishwa kisheria.

Anasema, sheria ziko kimya kwenye kuwajibisha vyama vinavyokiuka sharti la usawa wa jinsia katika uteuzi wa wanaowania kugombea nafasi mbalimbali za uchaguzi.

“Kwa upande wa Zanzibar, kifungu cha 49 cha sheria ya uchaguzi kimeweka kiwango cha 2,000,000 kwa mgombea urais, 200,000 kwa wagombea wa Baraza la Wakilishi na 30,000 kwa madiwani.

“Viwango hivi ni kikwazo kwa wanawake wenye uwezo wa uongozi ambao hawana uwezo kumudu kiwango hiki pamoja na gharama nyingine za kampeni,” anasema Profesa Ruth.

Wabunge wanawake

Anasema, sheria hakuipa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) msumeno wa kuwajibisha vyama vya siasa, ambavyo havizingatii msingi wa usawa kwenye uteuzi wa wanaowania kugombea nafasi kwenye uchaguzi katika ngazi zote.

Profesa Ruth anasema, wanazuoni wengi wanadai vyombo vya habari ni mhimili wa nne wa utawala katika uongozi wa nchi.

“Hii inatokana na uwezo wa vyombo vya habari kuathiri kwa kiwango kikubwa ajenda za wale wanaowania, kunyakua mamlaka ya uongozi wakati wa mchakato wa uchaguzi,” anasema.

Anasema, kimantiki, vyombo vya habari vinakuwa na jukumu la kuunganisha wale wenye kuomba ridhaa ya uongozi na wapiga kura katika kuhabarisha wapiga kura, ajenda za wale wanaowania uongozi na vilevile kuwasilisha madai na mataarajio ya wapiga kura na  wale wanaowania uongozi.

Amesema, vyombo vya habari ni nguzo muhimu kwenye kutekeleza  dhamira ya kujenga demokrasia shirikishi, kwenye kutetea haki za wanawake za kushiriki na kwenye kuonesha athari za ubaguzi wa jinsia katika ustawi wa jamii na ujenzi wa demokrasia shirikishi.

Anasema, vyombo vya habari vinaweza kuendeleza misingi ya ubaguzi kwenye uchaguzi kwa njia nyingi ikiwa ni pamoja na kutoa taswira hasi ya wanawake katika uongozi, katika matumizi ya lugha ya kuwadhalilisha na vilevile kwa kuacha kuwapa vipaumbele kwenye taarifa ya wanaowania nafasi hizo.

“Kutumia takwimu kuandika makala mbalimbali kuhusu ushiriki wa wanawake, mafanikio na changamoto. Vilevile taarifa kuhusu uwajibikaji wa vyombo vya habari katika kuhamaisha ushiriki wa wanawake katika uchaguzi,” amesema.

error: Content is protected !!