MASHAHIDI tisa na vielelezo kumi vitatumika katika kesi namba 407 ya 2022 ya kimtandao katika kundi la whassap inayokambili mwandishi wa habari za afya na uchunguzi wa gazeti la Raia Mwema Mary Victor na wenzake wawili Asha Mahita na Rogers Simeo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Akiahirisha kesi hiyo mapema wiki hii, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala Glory Nkwera alisema mashahidi tisa wataitwa kutoa ushahidi wao pamoja na vielelezo kumi vitatumika kama ushahidi mahakamani hapo Januari 17 kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.
Katika kesi hiyo Maria Victor anatuhumiwa na makosa matatu likiwemo la kutumia laini ya simu ambayo imesajiliwa kwa jina la mtu mwingine(Asha Mahita), na pia kutuma taarifa ya uongo kuhusu maradhi ya Covid katika kundi la waandishi la whassap.
Naye Asha Mahita na Rogers wanatuhumiwa kwa pamoja kushindwa kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mawasiliano(TCRA)mabadiliko ya umiliki wa laini hiyo ya simu yenye namba 0715166210.
Katika kesi hiyo Mary na wenzake wanawakilishwa na wakili kutoka Taasisi ya Sibaba Alex Masaba na wakili kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Anti Human Traffic and legal Initiatives Frank Mposso.
Akizungumza na Raia Mwema mahakamani hapo mapema hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la TATILI Godrey Mpandikizi alisema: “Tumeamua kuongeza nguvu ya kisheria tukishirikiana na wakili mwenzetu Alex Masaba kuhakikisha haki inatendeka;
“Mwandishi wa habari anapofanya wajibu wake kihabari hatakiwi kupata vitisho au misukosuko ya aina yoyote ile kwa sababu anatimiza moja ya jukumu lake, taasisi yetu kama mdau wa waandishi wa habari ina jukumu kubwa kumsaidia mwandishi wa habari au chombo chochote cha habari.
“Ndio maana taasisi yetu inatoa mchango wa hali na mali kisheria kuhakikisha mwandishi anakuwa salama na kuendelea kutimiza majukumu yake kama kawaida.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa tena Januari 17 mwakani(2023) na washitakiwa wote wamekana mashitaka na wapo nje kwa dhamana huku simu za baadhi ya washtakiwa, vitambulisho vyao ikiwemo simu mmoja wa wakurugenzi Mbaraka Islam zikiendelea kushikiliwa katika kituo cha polisi kati(central).
Leave a comment