August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mamilioni ya Rais Magufuli yazua balaa Mwanza

John Magufuli, Rais wa Tanzania alipokuwa kwenye ziara mkoani Shinyanga

Spread the love

JUMUIYA ya Maendeleo Kanindo (CDK) jijini Mwanza, imemtaka Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula, kuihoji serikali bungeni juu ya ahadi ya kutoa Sh 50 milioni kwa kila kijiji kwa ajili ya kukopesha wananchi walioungana katika vikundi vya maendeleo, anaandika Moses Mseti.

Agizo hilo kwa mbunge Mabula lilitolewa na Benjamin Masese, Katibu wa CDK, wakitaka kujua ahadi ya Rais Dk. John Magufuli aliyoitoa juu ya kutoa Sh. 50 milioni kwa kila kijiji wakati wa kampeni imefikia wapi.

Masese amesema tangu Rais Magufuli aahidi Sh 50 milioni huku akiwataka wananchi kuunda vikundi ili kupata mgawo huo, wananchi walihamasika lakini wanashangazwa kuona hakuna utekelezaji wowote uliopo.

“Uwepo wa CDK ni matokeo ya ahadi ya Rais Magufuli na swali lenu ni la msingi sana, hivyo tumtake mbunge wetu wa Jimbo la Nyamagana, Mabula, aihoji Serikali ili aje na majibu sahihi kwani naye alikuwa amesisitiza jambo hili.

“Hii Serikali inapaswa kuwa na utaratibu wa kutoa majibu sahihi, kwani Aprili 21, 2016, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Sera, Uratibu, Bunge la Walemavu, Antony Mavunde akiwa bungeni alimjibu Mbunge wa Viti Maalum, Halima Bulembo kwamba Serikali inatarajia kutoa Sh 50 milioni kila kijiji katika bajeti 2016/2017.

“Swali la msingi la Bulembo lilikuwa linafanana na lenu kwamba ahadi ya Rais Magufuli ya kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji imeishia wapi?, jibu lililotolewa ni hilo, sasa swali langu ni kwamba hiyo bajeti ya 2016-2017 bado ipo, kama tunavyojua hivi sasa wabunge wote wapo Dodoma kwa maandalizi ya kuanza kujadili bajeti ya 2017/2018, tunaomba Mabula aje na majibu kama fedha zilitengwa na zilitolewa vikundi gani,” amesema Masese.

Masese amesema kwa mujibu wa maelezo ya Mavunde bungeni, utaratibu wa kugawa fedha hizo unaandaliwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na vigezo ambavyo vitakuwa vikitumika katika kutoa mikopo na mitaji kwa vijana ni umri usiozidi miaka 35 ambavyo ni kujiunga na Saccos za vijana za wilaya na kuunda vikundi na kuvisajili kisheria.

Ayubu Kabati, Mwenyekiti wa CDK-Mwanza, amewataka wajumbe hao kuwa na subira wakati wanawasiliana na Maabula ili kupata majibu juu ya utekelezaji wa ahadi hiyo ambayo inaelezwa kwamba fedha zilitengwa katika mwaka wa bajeti ya 2016/2017 ambao unaelekea kumalizika Juni mwaka huu.

Kabati aliwataka wananchi wanaoishi Mtaa wa Kanindo kujiunga na CDK kwani bado idadi ya wanachama wanaotakiwa ndani ya jumuiya hiyo haijatimia, pia wameanza kukopeshana wenyewe kutokana na mtaji wao.

error: Content is protected !!