August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mvomelo waomba marekebisho ya skimu

Kilimo cha mpunga cha umwagiliaji

Spread the love

SERIKALI imeombwa kurekebisha na kupanua miundombinu ya skimu ya umwagiliaji maji iliyo chakavu kwenye kijiji cha Mlali, Mvomero ili iweze kusaidia wananchi wanaoikosa fursa ya kilimo cha umwagiliaji ambayo walikuwa wakiipata kipindi cha miaka ya 1980, anaandika Christina Haule.

Diwani wa kata hiyo, Frank Mwananziche amesema skimu hiyo ya umwagiliaji kwa sasa imekuwa chakavu licha ya kuwa miaka ya 1980 ilikuwa ikihudumia wakazi wengi wa eneo hilo na kufanya kuwa na kilimo cha mpunga makini kilichowainua kiuchumi wanavijiji wa kata hiyo.

Mwananziche amesema, licha ya watu kufanya shughuli za kibinadamu katika mto Mlali ambao ndio chanzo kikuu cha skimu hiyo na kufanya maji kupungua, uchakavu wa skimu hiyo unasababisha maeneo mengine ambayo maji yalikuwa yanafika kwa wakati, kutofika na kufanya shughuli za kilimo cha mpunga kushindwa kuendeshwa na kubakia kilimo cha mbogamboga.

Hata hivyo amesema, marekebisho ya skimu hiyo yatasaidia watu wengi kulima kufuatia kata hiyo kuwa na watu 21,159 kwa sasa tofauti na miaka 1980 kulikuwa na watu 3,000 pekee na kufanya kutumia skimu hiyo vyema katika kilimo cha mpunga na mazao ya mbogamboga tofauti na ilivyo kwa sasa ambapo watu wachache wameamua kuhodhi maeneo yenye maji na kuendelea na kilimo cha mbogamboga.

“Watu 2400 tu kutoka kwenye vijiji vichache vya kata hii ndio wanaonufaika na skimu hiyo, hivyo ikirekebishwa na kupanuliwa wanaweza wakaongezeka na kurejesha kilimo cha mpunga,” amesema diwani huyo.

Hata hivyo diwani huyo aliiomba serikali kuangalia namna ya kuboresha huduma za uhakika wa masoko hasa kwa wakulima wa nyanya ambao mara nyingi wamekuwa wakipoteza nyanya zao kufuatia kuoza baada ya kukosa kiwanda cha kuzipeleka kutengezwa kwa ajili ya uhifadhi wa muda mrefu (Tomato paste).

Naye Mkuu wa wilaya ya Mvomero, Mwalimu Utaly amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina nia njema na wananchi wake ambapo atakikisha anafuatilia suala hilo na kuona linarejesha na kuboresha huduma za skimu hiyo.

error: Content is protected !!