November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mambo tisa yaibuka kwenye mjadala mabadiliko mifumo ya elimu

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Richard Mabala

Spread the love

 

TAKRIBANI mambo tisa, yameibuka katika mkutano wa wadau, wa kujadili namna ya uboreshaji mitaala ya elimu nchini Tanzania. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mkutano huo wa kupokea maoni ya wadau kuhusu uboreshaji mitaala ya elimu ya awali, msingi na sekondari, umefanyika leo Ijumaa, tarehe 18 Juni 2021, katika Ukumbi wa Mlimani City mkoani Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako.

Masuala yaliyoibuka katika mkutano huo ni, uanzishwaji shule za ufundi, masomo yanayohusiana na ulemavu na ujuzi wa maisha, matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye ufundishaji, elimu ya dini kuwa ya lazima, walimu kupewa semina na utatuzi wa changamoto ya uhaba wa walimu.

Mengine ni, upatikanaji wa wakaguzi wa elimu wenye sifa, walimu wa shule za msingi kuwa na elimu ya Shahada (Degree), uanzishwaji mitaala inayokidhi matakwa ya sera ya sasa ya uchumi wa viwanda na bluu. Uanzishaji shule za ufundi za kikanda, kulingana na rasilimali zilizopo katika maeneo husika.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Richard Mabala, amependekeza lugha ya Kiswali, itumike katika kufundishia wanafunzi, ili kuwajengea uelewa zaidi.

“Lengo la elimu ni wanafunzi wajifunze, wapate ujuzi, maarifa. Na njia pekee kwa kupewa katika lugha wanayoielewa,”

“1982 wakati wa shule za sekondari zilikuwa chache, ulifanyika utafiti ulioonesha asilimia 10 ya wanafunzi, walikuwa wana uwezo wa kusoma vizuri lugha ya Kiingereza,” amesema Prof. Mabala na kuongeza:

“Sasa tumepanua elimu ya sekondari, lakini wanafunzi walio wengi hawana kingereza cha kutosha cha kuweza kusoma na kuelewa. Tunawanyima ujuzi, umahiri na stadi kwa sbabau hawana hiyo lugha.”

Mbunge Viti Maalumu asiye na chama bungeni, Nusrat Hanje, alishauri Serikali iandae mitaala inayokidhi soko la ajira la sasa, kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).

“Niwaombe wakati tunajiandaa kwenye hilo, tuwaalike ATE pamoja na TPSF. Sababu tunataka tujue soko la ajira linataka nini, tuandae product (bidhaa) gani inayohitajika kwenye soko la ajira. Sababu tuna andaa product isiyohitajika katika soko la ajira,” amesema Hanje.

Suala la masomo ya dini kuwa ya lazima, lilitolewa na Mkaguzi Mkuu wa Elimu Zanzibar,Dk. Rashid Abdul-Aziz Mukki, aliyeshauri lifanyiwe kazi katika maboresho hayo, ili kuwaandaa wahitimu wenye maadili.

Mkaguzi Mkuu wa Elimu Zanzibar,Dk. Rashid Abdul-Aziz Mukki

“Tuamue dini iwe lazima, yaani nani asiyetaka mwanamwe awe na maadili. Dini tumeiweka chaguo, sasa kwa upande wa Zanzibar sisi kwetu dini somo la dini ni lazima. Tukubaliane mtaala tunaoundaa sasa, dini iwe somo la lazima,” amesema Dk. Mukki.

Dk. Mukki amesema “sote tunakubaliana tunataka tuandae watu wema na wenye maadili, tunaogopa nini suala la dini kuwa somo la lazima?”

Mkaguzi huyo wa elimu Zabnzibar, amependekeza katika mabadiliko hayo, yaanzishwe masomo yanayohusu masuala ya rasilimali za baharini, ili kuwaandaa wahitimu watakaokidhi matakwa ya utekelezaji sera ya uchumi wa bluu.

“Tunapokwenda kwneye mtaala, Zanzibar sasa hivi iko katika kujiandaa na uchumi wa bluu, tuingizeni kwenye mitaala hii ya kawaida, tusingoje kufikia vyuo vikuu,” amesema Dk. Mukki.

Naye Fredy Sichizya, alipendekeza mabadiliko hayo yajumuishe uanzishaji wa michepuo ya masomo inayoendana na Sera ya Taifa ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Pia, Sichizya alipendekeza “ili kuweza kujitegemea, turudi katika shule zetu za awali, ziwe za ufundi kuanzia elimu ya msingi. Mitaala ielekeze shule zitegemee ukanda, tunapokuwa Ukanda wa Bahari ya Hindi kuwe na shule zinazohusika na uvuvi, hali kadhalika ufugaji na maneo ya kilimo.”

Abdulilah Omary, Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA)

Suala la kuwa na wakaguzi wa elimu wenye sifa, lilitolewa na Lilian Chovenya, aliyesema “mimi sijui kuna vigezo gani katika kuchagua wakaguzi wa elimu, wakaguzi wa elimu wengi mapolisi. Wanajenga hofu kwa walimu shuleni. Tunaomba wakaguzi wakichaguliwa, wapelekwe kozi ya kukagua mwalimu.”

Abdulilah Omary, kutoka Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), alipendekeza masomo kuhusu watu wenye ulemavu yaanzishwe.

“Katika elimu ya awali ni vyema kungekuwa na somo linalohusiana na ulemavu, nikiwa na maana kwamba watoto wetu wakitoka nyumbani, wawe na tafsiri tofauti za ulemavu hiyo inasaidia sana ushirikishwaji mpaka ngazi ya ajira,” amesema Omary.

error: Content is protected !!