May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli: Vyuo vya ufundi kujengwa kila mkoa

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania, imeahidi kujenga vyuo vya ufundi stadi vitakavyokuwa chini ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), katika kila mkoa, ili kuimarisha uchumi kupitia sekta ya viwanda nchini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kagera … (endelea).

Ahadi hiyo imetolewa leo Jumatatu tarehe 18 Januari 2021, mkoani Kagera na Rais wa Tanzania, John Magufuli, wakati anafungua majengo ya Shule ya Sekondari ya Wavulana Ihungo pamoja na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha VETA mkoani humo.

“Uchumi wa nchi yoyote unategemea viwanda, hata hivyo, itakuwa ni ndoto kufikia azma hiyo bila kuwekeza nguvu zetu katika kuimarisha kwenye elimu ya ufundi stadi. Kama mjuavyo elimu ya ufundi ni msingi mkuu wa ustawi wa ujenzi wa viwanda,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, mkakati huo wa ujenzi wa vyuo vya VETA katika kila mkoa, umeashaanza kutekelezwa.

“Kwa lengo la kupanua wigo wa elimu ya ufundi na kufikia azma ya Serikali kujenga vyuo vya VETA kila mkoa na wilaya, tunajenga vingine vipya 33 ambapo vinne vya ngazi ya mkoa na 29 ngazi ya wilaya, vitakapo kamilika vitadahili wanafunzi 65,640,” amesema Rais Magufuli.

Sambamba na hilo, Rais Magufuli amesema, vyuo vya VETA vimeongezeka kutoka 672 vilivyokuwa mwaka 2015 hadi kufikia 712.

Kuhusu ujenzi wa Chuo cha VETA Kagera, Rais Magufuli amesema, ukikamilika chuo hicho kitadahili wanafunzi 800 hadi 1,000 kwa mwaka.

Aidha, Rais Magufuli amemuagiza Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jaffo kujenga kwa kiwango cha lami, barabara inayoingia chuoni hapo yenye urefu wa kilomita 10.

Na kuwaomba wananchi wanaokaa karibu na barabara kuytoa ushirikiano kwa Serikali ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati.

“Na nimeagiza barabara kutoka chuo cha VETA kinapojengwa ambapo kuna kilomita kama 10, ijengwe nayo kwa kiwango cha lami. Ila nitawaomba wakazi wa eneo hili wakubaliane na Serikali wakati tunaanza kupanua barabara,” amesema Rais Magufuli.

Kiongozi huyo wa Tanzania amesema, ujenzi wa chuo hicho unafadhiliwa na Serikali ya China kwa gharama ya Sh. 22 bilioni, utakamilika mwaka huu.

“Serikali ya China ilitusaidia Sh.22 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki kikubwa, na kimeanza kujengwa ambacho tunategemea mwaka huu utakamilika,” amesema Rais Magufuli.

Akielezea ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Ihungo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema shule hiyo imepanuliwa na kwmaba ina uwezo wa kuchukua wanafunzi wengi.

“Kabla ilikuwa inachukua wanafunzi 640, kwa maelekezo yako ulituelekeza tuijenge ichukue wanafunzi wasiopungua 1,000. Tumetekeleza malekezo hayo na shule hii inauweo wa kuchukua wanafunzi 1,152 kutoka 640,” amesema Prof. Ndalichako.

Waziri huyo wa elimu amesema, shule hiyo imekarabatiwa baada ya majengo yake kuharibiwa vibaya ya tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera tarehe 10 Septemba 2016.
“Tarehe 10 Septemba 2016 tulipata tatizo la tetemeko Mkoa wa Kagera ambalo liliathiri miundombinu ya makazi ya wananchi pamoja na Serikali, shule iliharibika majengo mengi yalitetekea, rais ulituagiza tuijenge na tuhakikishe tunaongeza idadi ya wanafunzi,” amesemaProf. Ndalichako.

Prof. Ndalichako amesema ukarabati huo umefadhiliwa na Serikali ya Uingereza iliyotoa Sh. 6.1 bilioni na Serikali ya Tanzania iliyotoa Sh. 4.8 bilioni.

Hata hivyo, Prof. Ndalichako amesema, Serikali inatekeleza mradi wa ukarabati wa shule kongwe 89, ambapo hadi sasa shule 84 zimeshakarabatiwa na zilizobaki ziko katika hatua za mwisho.

error: Content is protected !!