ALIYEKUWA kiungo wa klabu ya Arsenal na timu ya Taifa ya Ujeruman, Mesut Ozil amejiunga na klabu ya Fenerbahce ambayo anakipiga mtanzania Mbwana Samatta inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uturuki. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Ozil ambaye alitupwa nje ya kikosi cha Arsenal mwanzo wa msimu na kocha Mikel Arteta mara baada ya kutokuwa katika mipango yake toka alipochukua mikoba ya kukinoa kikosi hiko.
Mapema jana mchezaji huyo aliweka picha akiwa kwenye ndege na familia yake kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram akionesha anaelekea nchini Uturuki na saa chache baadaye aliweka picha akiwa ameshika skafu ya klabu ya Fenerbahce.

Klabu hiyo pia baadae ikamtambulisha Ozil kama mchezaji mpya kwenye kikosi chao mara baada ya kumsajili kwenye dirisha dogo la usajili mwezi Januari.
Ozil atakwenda kuungana na nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars,’ Mbwana Samatta ambaye anaongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo toka alipojiunga nao kwenye dirisha kubwa la usajili mwanzoni mwa msimu wa 2020/21.
Huenda kujiunga kwa Ozil ndani ya Fenerbahce kutafanya Samatta kung’aa zaidi kutokana na umahili wake wa kupiga pasi za mwisho za mabao anapocheza nyuma ya mshambuliaji.
Leave a comment