December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli ataja mrithi wake 2025, Lukuvi na Kabudi ‘out’

Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli amesema, mtu atakayerithi mikoba yake baada kutoka madarakani mwaka 2025, hatakuwa na umri mkubwa zaidi yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Kauli hiyo ameitoana leo Jumatatu tarehe 16 Novemba 2020 wakati anazungumza katika hafla ya uapisho wa viongozi aliowateua hivi karibuni, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Viongozi walioapishwa ni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyemteua na kuthibitishwa na Bunge tarehe 12 Novemba 2020. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi ambao aliwateua tarehe 13 Novemba mwaka huu.

Rais Magufuli amewashauri wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaotaka kusaka ridhaa ya chama hicho kugombea Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kuhakikisha kwamba hawamzidi umri.

Huku akiwataka wanaomzidi umri kutopoteza muda wao kuusaka urais wa Tanzania kwa kuwa hawatafanikiwa.

“…tukapendekeze kwenye kamati kuu tuchague rais anayenizidi umri mimi? huo ndio ukweli, maneno mengine yanaumiza. Nataka niwaleze mkajitayarishe kisaikolojia kusudi msipoteze hela zenu,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema hata yeye alikabidhiwa madaraka na Rais wa Serikali ya awamu ya nne, Jakaya Kikwete, ambaye hakumzidi umri.

“Kikwete wakati anaondoka alisema hawezi kuacha rais anayezidi umri wake, sasa niiangalie mimi nina umri gani wakati namaliza, ujipimie kwenye umri pale,’ amesema Rais Magufuli huku akishangiliwa na wageni waliopo.

Rais Magufuli aliyezaliwa tarehe 29 Oktoba 1958 sasa ana miaka 62 huku mwaka 2025 akiwa anaondoka madarakani atakuwa na miaka 67.

Kiongozi huyo wa Tanzania aliingia madarakanitarehe 5 Novemba 2015 akipokea kijiti hicho kutoka kwa Rais Kikwete, baaada ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka huo.

Wakati anaingia madarakani, Rais Magufuli alikuwa na miaka 57 huku aliyemwachia Ikulu, Rais mstaafu Kikwete alikuwa na miaka 65.

Kwa sasa Rais Magufuli anaendelea na muhula wa mwisho wa uongozi wake kwa mujibu wa Katiba baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020 na kuapishwa kuiongoza Tanzania tarehe 5 Novemba 2020 jijini Dodoma.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, Rais Magufuli alitangazwa mshindi wa kiti cha Urais wa Tanzania na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) kwa kupata kura asilimia 84 huku aliyekuwa mpinzani wake wa karibu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu akipata kura asilimia 13.
Akikazia hoja yake hiyo, Rais Magufuli amewaorodhesha baadhi ya makada wa CCM ambao hawatakidhi sifa hizo, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi.

“Nataka niwaeleze mkajitayarishe kisaikolojia kusudi msipoteze hela zenu, hata wewe Kabudi huwezi kuwa rais, najua haya maneno ni magumu lakini ndio ukweli,” amesema Rais Magufuli.

Mbali na Prof. Kabudi, Rais Magufuli amemtaja aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuwa yupo kwenye kundi la watu ambao hawataweza kupata nafasi ya kuirithi mikoba yake.
Licha ya kwamba, Lukuvi ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho Taifa (NEC).

“Hata mimi sikujua kama nitakua rais sababu katika miaka yangu 20 ya ubunge na uwaziri sikuwahi kuomba hata ujumbe wa NEC, wajumbe wa NEC walikuwa kina Lukuvi lakini urais hakuupata na sina uhakika kama ataupata. Sasa ana miaka zaidi ya 60 na kitu,” amesema Rais Magufuli.

Mwenyekiti huyo wa CCM amesema chama hicho kinapaswa kuwa na mgombea wa urais kijana ambaye atakidhi matakwa ya wapiga kura wengi ambao ni vijana.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli amewaeleza waliohudhuria kwamba, “Najua mmenyamaza kwa hiyo unawezekana umekaa na jirani yako amabye ndio akawa rais kijana zaidi.”

Rais Magufuli amesema, hata yeye alishinda katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020 kwa kuwa alipigiwa kura na vijana.

Rais huyo wa Tanzania wa awamu ya tano amesema, hata Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi alishinda kiti hicho kwa kuwa alikuwa kijana na wapiga kura wengi walikuwa vijana.

Rais Magufuli amesema viongozi wa Serikali watakao vuka rika hilo akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela wataendelea kuheshimiwa kwa utumishi wao, kwa kuwa hawataweza kuwa marais.

“Yaani Malecela tumpendekeze rais wa Tanzania? Haiwezekani, ameshakuwa mstaafu tuna mheshimu, tunampenda lazima tuseme ukweli,” amesema Rais Magufuli.

error: Content is protected !!