Tuesday , 21 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Magufuli atoa sababu kumteua haraka Kabudi, Mpango
Habari za Siasa

Magufuli atoa sababu kumteua haraka Kabudi, Mpango

Spread the love

RAIS wa Taznania, John Pombe Magufuli ameeleza namna ‘alivyokoshwa’ na utendaji wa Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikian wa Afrika Mashariki pia Dk. Philip Mpango, Waziri wa Fedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Amesema, mawaziri hao katika serikali yake iliyopita, wamefanya kazi ya kutukuka hivyo amelazimika kuanza nao kabla ya kuteua baraza lake jipya la mawaziri.

“Hawa wawili sio kwamba ni maarufu sana kuliko wengine waliobaki, miaka ya nyuma niliwateua hawakuwa na majimbo na niliwaambia kwamba waende kwenye majimbo au waende walikotoka wakaenda kwenye majimbo,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alifanya uteuzi wao tarehe 13 Novemba 2020, siku chache baada ya kuapishwa tarehe 5 Novemba 2020, kuongozwa ngwe yake ya pili.

Akizungumza katika hafla ya kumwapisha Kasim Majaliwa, Waziri Mkuu na mawaziri hao leo Jumatatu tarehe 16 Novemba 2020, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Rais Magufuli amesema, amewateua tena kwa kuwa walimudu majukumu yao vizuri.

Amesema, kwa kuwa alilidhishwa na utendaji kazi wa Dk. Mpango na Prof. Kabudi, aliwashauri wakagombee katika majimbo kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka huu.

Akimzungumzia Dk. Mpango, Rais Magufuli amesema alimteua tena awe Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuwa katika baraza lililopita alitimiza majukumu yake vizuri na kuanikiwa kuivusha Tanzania kutoka katika nchi masikini hadi kufikia uchumi wa kati.

Rais Magufuli amesema, Dk. Mpango kabla hajateuliwa kuwa Waziri wa Fedha alifanikiwa kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya Serikali alipokuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Ndio maana nikaangalia huyu Mpango kabla sijamteua alikuwa kamishna wa TRA alikuwa mtu wa kwanza kukusanya Sh.850 bilioni hadi Sh.1.2 trilioni.”

“Nikamteua kuwa waziri wa fedha na uchumi wetu uliendelea kupanda akatutoa uchumi wa chini mpaka wa kati. Nikasema nimruidshe ndio maana nikamrudisha,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, “lakini nikaona sababu nitachelewa kidogo kuwa na baraza la mawaziri na ninyi wabunge lazima mlipwe mishahara. Lazima tutafute fedha za kulipa wafanyakazi na Watanzania, lazima tuwe na miradi ya maji sababu yenyewe haisimami, nikasema lazima tuwe na waziri wa fedha sababu fedha tutazihitaji haziwezi kusubiri miezi mitatu au minne,” amesema Rais Magufuli.

Kuhusu Waziri Kabudi, Rais Magufuli amesema amemteua tena kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa kuwa alimudu kazi yake vizuri katika baraza lililopita.

Kiongozi huyo wa Tanzania amesema aliamua kuwahi kumteua Waziri wa Mambo ya Nje ili nchi iwe na msemaji katika masuala ya kimataifa.

“Niliona Wizara ya mambo ya nje tutakosa wa kutusemea tutaendelea kutukanwa, watu wakatengeneza majambo yao tutakosa majibu, nikasema huyu sababu alimudu kazi yake ngoja aendelee kuwa waziri wa mambo ya nje,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema aliamua kufanya uteuzi wa mawaziri hao wawili kwa kuwa wizara zao ni muhimu katika kufanikisha shughuli za nchi ziendelee wakati anafanya uchambuzi wa wabunge atakaowateua kuwa mawaziri.

Dk. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na MIpango Tanzania

Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais amesema, Rais Magufuli amewateua tena mawaziri hao kwa kuwa aliwanyoosha katika awamu iliyopita.

“Leo nataka nikupe siri ndogo, rais sisi ulioturudisha imani kubwa haikuwa rahisi kivile, tulipoanza nawe ilikuwa ngumu. Tulikuwa tunalia kila siku lakini uliendelea kutunyoosha, mheshimiwa Rais tumenyooka,” amesema Mama Samia.

Mama Samia amesema katika miaka miwili ya mwanzo ya uongozi wa Rais Magufuli, walikuwa na wakati mgumu kutambua maono yake, lakini katika miaka iliyofuata walinyooka kitendo kilichopelekea awaamini na kuwateua tena.

Mama Samia amesema, kutokana na uzoefu wa mawaziri hao, Dk. Mpango atahakikisha anakusanya fedha za kutosha za kuendesha nchini, wakati Prof. Kabudi akihakikisha uhuru wa Tanzania hauingiliwi na wafadhili.

‘Na mimi nikuahidi tutachapakazi kutimzia kurasa 303 tulizopita kunadi kwa wananchi, mwenye fedha amesema hatakuwa na mchezo atakwenda azikusnaye tuchapekazi,”

“Anayesughulikia na mambo ya nje hatakuwa na mchezo atakwenda kuhakikisha uhuru Watanzania unabaki, kwamba Tanzania tufanye mambo yetu tukiwa huru anayekuja na msaada tutampokea na si kwamengine,” amesema Mama Samia.

Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesifu mawaziri hao wawili kwamba ni watendaji wazuri.

“Kabudi na Mpango wote walikuwa ni wenzangu nawafahamu ni watendaji wazuri na wanastahili kwa nafasi hizi ambazo wameminiwa,” amesema Rais Mwinyi.

Viongozi ambao Rais Magufuli amewarudisha tena katika wadhifa wao ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Adelardus Kilangi, Waziri Majaliwa, Prof. Kabudi na Dk. Mpango.

Hivi karibuni Rais Magufuli aliwatoa wasiwasi wateule wake wengine wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya na watumishi wnegine kwamba hatotengua teuzi zao.

Isipokuwa atafanya mabadiliko katika nafasi za mawaziri na manaibu waziri.

Hata hivyo, ameahidi kutengua teuzi za watumishi wa umma na watendaji watakaokuwa wazembe katika utekelezaji wa majukumu yao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia aagiza iundwe kamati ya pamoja ya Mawaziri mradi wa BBT

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza mawaziri kuunda kamati...

Habari za Siasa

Rais Samia apangua makatibu tawala mikoa, ateua Kamishna DCEA

Spread the loveALIYEKUWA Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Gerald...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

M/kiti bodi ya wadhamini Chadema afariki dunia

Spread the loveMWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Demokrasia na...

Habari za Siasa

Zitto: Nikifa Ado atavaa viatu vyangu

Spread the love  KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe...

error: Content is protected !!