JOHN Magufuli, Mgombea Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameahidi kuimarisha mifumo ya kisera na kisheri kwenye sekta ya madini ili Watanzania wote wanufaike na rasmiliamli hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Shinyanga … (endelea).
Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo leo Alhamisi tarehe 3 Septemba 2020 wakati akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020/25 katika mkutano wa kampeni za Urais mkoani Shinyanga.
Amesema mabadiliko hayo yatawawezesha Watanzania kunufaika na utajiri wa madini, kwa kuwa watapewa kipaumble katika shughuli za uchimbaji madini.

“Ukurasa wa 105 unazungumzia juu ya masuala ya madini, kuimarisha mifumo ya kisera na kisheria ili kuwezesha wananchi wa Taifa kwa ujumla kunufaika na utajiri wa madini na rasilmali zao.”
“Tunataka madini haya yawanufaishe, ndio maana tunaruhusu wachimbe wenyewe,” amesema Magufuli.
Wakati huo huo, Magufuli ameahidi kuboresha sekta ya kilimo mkoani Shinyanga na Tanzania kwa ujumla, ikiwemo kutekeleza ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo .
“Katika ukurasa wa 44 wa Ilani ya CCM, unazungumzia juu ya kujenga vituo vya kuchakata na kuhifadhi mazao katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Iringa, Kagera, Manyara, Mara Mbeya, Tabora, Morogoro, Mtwara na Shinyanga,” ameahidi Rais Magufuli.
Leave a comment