Friday , 2 June 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Maganja wa NCCR-Mageuzi abainisha vipaumbele 10 ikiingia Ikulu
Habari za Siasa

Maganja wa NCCR-Mageuzi abainisha vipaumbele 10 ikiingia Ikulu

Spread the love

CHAMA cha NCCR-Mageuzi nchini Tanzania leo Jumamosi tarehe 5 Septemba 2020 kimezindua rasmi kampeni zake za Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Zakhiem-Mbagala jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi wa NCCR-Mageuzi akiwemo Mwenyekiti wake, James Mbatia.

Katika uzinduzi huo, Chama cha NCCR-Mageuzi kimewanadi wagombea wake katika Kiti cha Urais wa Tanzania na Makamu wa Rais. Yeremia Kulwa Maganja akiwa mgombea Urais huku Haji Ambar Khamis akiwa mgombea wake mwenza.

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na Angelina Mutahiwa, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria uzinduzi huo.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Maganja ametaja vipaumbele vyake 10 atakavyovifanyia kazi endapo atachaguliwa na Watanzania ikiwemo upatikanaji wa katiba mpya, elimu, mwafaka wa kitaifa, afya na ustawi wa jamii, mazingira na makazi, uhuru wa vyombo vya habari na asasi za kiraia.

Vipaumbele vingine ni usawa wa kijinsia, uchumi, ulinzi na usalama na vita dhidi ya rushwa.

Maganja amesema, endapo atafanikiwa kushinda, Serikali yake itaweka mkazo katika uboreshaji wa huduma za afya na elimu.

“Kuhusu afya na elimu, tutawekeza nguvu hizo huko sehemu nyingine tutaachia sekta binafsi ambapo serikali itawawezesha,” amesema Maganja.

Akifafanua zaidi sera yake kuhusu sekta ya elimu, Maganja amesema, atabadili mfumo wa elimu kwa kuanzisha elimu kazi ili wahitimu wawe na sifa za kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

“Tutaipa elimu yetu impe mtoto uwezo wa kuwa na ujuzi na maarifa yaani elimu kazi, tutabadili mfumo wa elimu wa namna ya kufundisha watoto ili iwe elimu kama ya mataifa yaliyofanikiwa kupitia utoaji elimu kazi.”

“Mafunzo anayopatiwa mtoto yatakuwa yanayompa ujuzi wa kutatua matatizo ya maisha yake na maarifa yatakayomfanya awe na ushindani uliosawia na watu wanaosoma mataifa mengine,” amesema Maganja.

Maganja amesema, sera ya elimu bure itaakuwa ni takwa la Kikatiba.

“Katiba tutakayoandika cha kwanza ndani yake elimu itakuwa takwa la lazima, mtoto anapozaliwa analindwa na Katiba kuwa na elimu mpaka atakapopata ujuzi utakaomumwezesha kujitegemea au kuajiriwa. Hakuna hadithi ya karo kuanzia mtoto mdogo hadi anapata ujuzi na hii itaandikwa kwenye katiba,” amesema Maganja.

Maganja ameahidi kuleta mapinduzi ya kilimo, kutoka katika kilimo cha kujikimu hadi kuwa kilimo cha biashara.

“NCCR tumefanya utafiti wa kutosha kuhusu kilimo. Asilimia 70 ya Watanzania wameajiriwa na kilimo. Tutakibadili kilimo tutakitoa kwenye kilimo cha kujikimu cha kutumia jembe na pembejeo hatarishi, kwenda kwenye kilimo cha kuwapa faida kwa kuzalisha kwa wingi kwa maana viwanda vitakuja vyenyewe. Viwanda huwa haviitwi,” amesema Maganja.

Kuhusu sekta ya biashara, Maganja ameahidi kuboresha sheria za kodi ili kuondoa kodi zinazokandamiza wafanyabiashara.

“Kuna utitiri wa kodi zisizo na tija . Nitatunga sheria rafiki zitakazowezesha mfanyabiashara kujenga mtaji. Naamini kupitia sekta binafsi watu watakuza mitaji, wataajiri watu na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa na uchumi wa kati,” amesema Maganja.

Maganja ameahidi kuziunganisha sera za vyama vya siasa ili Taifa liwe na sera moja.

“Baada ya uchaguzi sera za vyama vyote tutaziweka mezani, nitaunda timu ya kupitia sera hizo na kuunda sera za kitaifa. Chombo hicho kitakuwa cha kitaifa ili kila rais anayekuja asije na sera zake afuate sera ya kitaifa,” amesema Maganja.

Maganja amesisitiza “Sera zitakazokuwa zinapitishwa ni sera za vyama zitakazotengeneza sera moja ya taifa, miaka yote tunarudi nyuma sababu kila anayekuja anakuja na sera zake. Leo huyu anakuja na sera za ubinafsishaji, akija mwingine anakuja na sera ya biashara, wapi na wapi, Serikali ikafanya biashara? Matokeo yake hatusongi mbele.tunarudi nyuma.”

Kwa mujibu wa ratiba ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2020 iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kampeni za uchaguzi huo zilianza tarehe 26 Agosti 2020 na zitafungwa tarehe 27 Oktoba 2020.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Lusinde: CCM hatuliachii ng’o jimbo la Moshi Mjini

Spread the loveMJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Livingston...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar: Bakharesa hajavamia shamba letu

Spread the love  IKULU Visiwani Zanzibar, imeeleza kuwa eneo la kiwanda cha...

Habari za SiasaTangulizi

Zanzibar watangaza rasmi kuwa shamba la Razaba ni mali yao

Spread the love  SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imetangaza rasmi kwamba shamba...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Mwinyi azindua Kamati ya Maridhiano Visiwani

Spread the love  RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Hussein...

error: Content is protected !!