Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Majaliwa: Bilioni 577 zatekeleza miradi Arusha, mchagueni Magufuli
Habari za Siasa

Majaliwa: Bilioni 577 zatekeleza miradi Arusha, mchagueni Magufuli

Spread the love

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli imetoa Sh.577.53 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara jijini Arusha. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Majaliwa ameyasema hayo leo Jumamosi tarehe 5 Septemba 2020 alipohutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Relini jijini Arusha baada ya kumuombea kura Rais Magufuli na mgombea ubunge jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo na wagombea udiwani wa CCM.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu imesema, Majaliwa amesema kati ya fedha hizo, Sh.1.3 bilioni zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Arusha ambapo jengo la wagonjwa ya nje (OPD) limekamilika na ujenzi wa jengo la akina mama unaendelea.

“Jumla ya Sh.1.5 bilioni zimetolewa kwa Jiji la Arusha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya vya Muriet, Kaloleni na Moshono ambapo ujenzi wake umekamilika na wananchi wanaendelea kupatiwa huduma.”

Majaliwa amesema, mbali na ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, pia Serikali imetoa Sh.3.8 bilioni kwa ajili ununuzi wa dawa na vifaa tiba kwa kipindi cha 2015/2016–2019/2020 katika jiji la Arusha, upatikanaji wa dawa umefikia asilimia 98.

Amesema Serikali imetoa Sh.2.14 bilioni kwa ajili ya kugharamia shughuli za ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu katika shule za msingi 48 jijini Arusha.

“Sh.4.68 bilioni zimetolewa katika shule za sekondari 29 kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa Wakuu wa Shule.”

Pia, waziri mkuu amesema, Sh.1.03 bilioni zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya madarasa na vyoo kwa shule mbalimbali za msingi jijini Arusha ikiwemo Olasiti, Daraja II, Oloirien na Sokoni I.

Akizungumzia kuhusu shule za sekondari, waziri mkuu amesema, Serikali imetoa Sh.4.68 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa, mabweni, vyoo na majengo ya utawala ikiwemo shule za Suye, Muriet, Lemara, Sorenyi, Arusha na Korona.

“Jiji la Arusha linakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, hivyo Serikali imetoa jumla ya Sh.520 bilioni kwa ajili ya mradi wa majisafi jiji la Arusha ambao utahudumia Jiji lote la Arusha. Utekelezaji wake umefikia asilimia 52.”

Amesema Sh.38.4 bilioni zimetolewa kupitia TARURA katika kipindi cha 2015/2016 – 2019/2020 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami na madaraja kwa jiji la Arusha ukiwemo ujenzi wa barabara ya Oljoro – Muriet yenye urefu wa kilomita 2.8.

Amesema, barabara nyingine ni za Kisongo Bypass kilomita 3.4, barabara ya Sokoine –Muriet Meidimu urefu wa kilomita 8.5, barabara ya Njiro kilomita 2.8, barabara ya Ngarenaro kilomita 4.1 na ujenzi wa barabara ya Sombetini kilomita 2.0.

“Barabara ya Arusha – Holili/Taveta. Ujenzi wa sehemu ya barabara kutoka Sakina hadi Tengeru, kilomita 14.1 na ujenzi wa barabara ya mchepuko wa kusini (Southern-bypass), kilomita 42.41 ambazo zinajengwa na TANROADS (Wakala wa Barabara Tanzania) zitahudumia Jiji lote la Arusha na Halmashauri za Wilaya Arusha na Meru.”

Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Arusha kumchagua Rais Magufuli kwa kuwa ana uwezo mkubwa wa kusimamia mambo yanayowagusa wananchi na ametekeleza vyema Ilani ya CCM ya mwaka 2015 kwa vitendo na sasa anakuja na Ilani mpya iliyosheheni mambo mengi ya maendeleo.

Waziri mkuu ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano Watanzania wakiwemo wakazi wa mkoa huo wa Arusha wamenufaika kutokana na miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo imejengwa nchini ikiwemo ufufuaji wa usafiri wa treni ya Dar es Salaam hadi Arusha ambao ulikuwa umesimama kwa takribani miaka 30.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia kutunukiwa udaktari wa heshima Uturuki

Spread the loveBaraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili...

error: Content is protected !!