January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mafao ya wastaafu, vitambulisho vya NIDA vyaibuliwa bungeni

Spread the love

 

WABUNGE wa chama tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamehoji mikakati ya Serikali kutokomeza changamoto ya ucheleweshaji wa mafao ya wastaafu na vitambulisho vya uraia, vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Anaripoti Glory Massamu, TUDARCo … (endelea).

Maswali hayo yamehojiwa leo Alhamisi, tarehe 2 Septemba 2021, bungeni jijini Dodoma, kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Swali la wastaafu kucheleweshewa mafao yao, liliulizwa na Mbunge Viti Maalum, Janejelly Ntate, aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani kuhakikisha wastaafu wanapata stahiki zao kwa wakati.

“Watumishi wanaostaafu kupata mafao kumekuwa na usumbufu mkubwa, katika mafao ya watumishi wanapostaafu kuchukua muda mrefu. Je, nini tamko la Serikali juu ya kuwawezesha wastaafu wetu ambao wametumikia Taifa kwa juhudi, kupata mafao kwa wakati,” amesema Ntate.

Akijibu swali hilo, Waziri Majaliwa, Serikali imeendelea kuratibu namna ya kuwalipa wastaafu kwa wakati, kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumsishi wa Umma (PSSSF).

“Nikiri bado kuna wachache hawajapata mafao yao kwa muda, lakini Serikali inaendelea kulipa wastaafu kadiri inapopata fedha,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema hadi kufikia Aprili 2021, Serikali imelipa wastaafu mafao ya Sh.172 bilioni.

“Aprili tumelipa zaidi ya Sh. 172 bilioni kwa wastaafu na tunaendelea kutenga fedha kulipa wastaafu, lakini pia mfuko huu umerahisisha namna ya kuwafikia wastaafu. Tumefungua ofisi za PSSSF ili wastafu waweze fika mkoani kutatua changamoto zao,” amesema Majaliwa.

Naye Mbunge wa Kilombero, Abubakar Asenga, aliihoji Serikali kwa nini isiunganishe mifumo ya kielektroniki ya Wakala wa Usajili, Ufisili na Udhamini (RITA), NIDA na Idara ya Uhamiaji, ili kumrahisishia mwananchi kupata kitambulisho cha uraia.

“Kumekuwa na ucheleweshaji vitambulisho vya utaifa kwa baadhi ya maeneo, kutokana na kutokuwepo mtiririko wa kujiridhisha wa taarifa za wananchi,” amesema Asenga na kuongeza:

“Serikali haioni umuhimu kuunganisha taasisi ya RITA, NIDA na uhamiaji kidigitali ili mtoto anapozaliwa taarifa zake zitumiwe na kutumika katika kutengeneza kitambulisho.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Akimjibu Asenga, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali haiwezi kuunganisha taasisi hizo kwa kuwa utendaji wake unajitegemea.

“Kwa hiyo RITA kinaweza kutoa cheti cha kuzaliwa hata kama sio Mtanzania, inatoa kitambulisho kwa yeyote anayezaliwa Tanzania, lakini kitambulisho cha taifa kinatolewa kwa Watanzania,”

“Kuunganisha kwa wakati mmoja, yako maeneo huwezi kuunganisha kama unavyofikiria lakini wanaweza kutoa taarifa kama chombo kimoja kinahitaji taarifa kutoka chombo cha pili,” amesema Waziri Majaliwa.

Amesema, kinachochelewesha vitambulisho hivyo kutolewa kwa wananchi ni zoezi la uhakiki ili kujiridhisha vinatolewa kwa Watanzania na sio raia wa kigeni, kwa ajili ya kulinda usalama wa nchi.

“Kwenye mikoa nilikopita, urasimu unazungumzwa kwamba wanachelewa kutoa vitambulisho vya NIDA, ni kweli. Kwa sababu utoaji kitambulisho cha Taifa, hii inajikita zaidi kwenye usalama wa nchi huwezi kumtambua yeyote anayekuja nchini bila kujiridhisha kama Mtanzania ukampa kitambulisho,” amesema Majaliwa na kuongeza:

“Kwa hiyo lazima kutakuwa na kuchelewa kidogo, kama kuna urasimu ni wa aina hiyo kujiridhisha huyu aliyeomba ni Mtanzania au wa kutoka nje ili maamuzi yafanyike. Kwa hiyo huo sio urasimu bali ni kuhakiki kwa kina ili cheti cha NIDA kitolewe kwa Watanzania tu.”

error: Content is protected !!